MBUNGE wa Jimbo la Dodoma mjini Mhe. Anthony Mavunde ameanza kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo katika shule za Msingi na Sekondari za Jiji la Dodoma akilenga kukuza michezo na kuwaandaa wanafunzi wenye vipaji kuanzia ngazi ya chini.
Mavunde ameyasema hayo katika shule ya Sekondari Dodoma wakati alipokuwa akikabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya shilingi 3,000,000 kwa wanafunzi wanaounda timu ya Jiji la Dodoma katika mashindano ya UMISETA ngazi ya Mkoa ambapo aliwahakikishia wanafunzi hao kuwawekea miundombinu bora katika viwanja vya shule zao wanavyotumia kwa ajili ya michezo mbalimbali.
“Nimefurahi kujumuika hapa nanyi siku ya leo ikiwa ni hafla fupi ya kuwakabidhi vifaa vya michezo na kuwatakia kila la kheri katika mashindano yenu ya UMISETA ngazi ya mkoa.
Ningependa kuona Jiji la Dodoma linakuwa mbele katika kila jambo ikiwemo michezo, hivyo ni imani yangu kwamba mtafanya vizuri katika mashindano haya ya mkoa;
Ninaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja katika shule zenu kwa kuweka magoli ya chuma ya chuma na kukarabati baadhi ya viwanja. Awamu ya kwanza naanza na shule 20 za msingi na sekondari na baadaye tutamalizia katka viwanja vilivyobaki” Alisema Mhe. Mavunde.
Aidha, Mhe. Mavunde aliwatakia kila kheri timu ya UMITASHUMTA ya mkoa wa Dodoma ambayo inajiandaa na safari ya kuelekea Mtwara kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya Taifa na kuahidi kuwapa kiasi cha shilingi Milioni 2 endapo watashinda walau michezo mitano kati ya michezo yote watakayoshiriki.
Naye Mwalimu Upendo Rweyemamu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma, alimshukuru Mhe. Mavunde kwa kufadhili vifaa vya michezo kwa timu za wanafunzi za Jiji la Dodoma kila mwaka na amemuahidi ushindi katika michezo yote ili kulinda hadhi na heshima ya Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.