Na. Asteria Frank, DODOMA
Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Relini, Kata ya Kizota, Lizi Edward amshukuru Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kuwanufaisha wananchi kupitia miradi ya maendeleo ya elimu kwa kuanzisha ujenzi wa Shule ya Msingi Mbuyuni kwa lengo la kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na serikali katika Kata ya Kizota.
“Kipekee nipende kumshukuru Mhe. Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde kwa kutuletea na kutusapoti kuanzisha ujenzi wa shule ya Mbuyuni ambapo kwa kushirikiana na nguvu za wananchi tumefanikiwa kujenga madarasa sita na ofisi mbili ambapo bado haijakamilika. Pia tunaishukuru serikali kwaajili ya kutupatia mradi wa kituo cha afya kwaajili ya kutoa huduma na kuboresha afya za wananchi” alisema Edward.
Kwa upande wake Mwalimu wa shule ya Msingi Mahungu, Mwl. Donatus Gagula, alisema kuwa shule imeanza kujengwa mwezi Oktoba 2024, kupitia mradi wa BOOST na inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi tarehe 22 Aprili baada ya likizo ya robo muhula. “Hii shule imejengwa kwaajili ya kuwasaidia wanafunzi baada ya serikali kubaini kwamba kuna maeneo ambayo yanahitajika shule zijengwe kwa maana kuna wanafunzi wanatoka sehemu za umbali mrefu kutoka katika makazi yao. Hivyo, serikali ikaamua kwamba ijenge shule hii mpya ya Msingi Mahungu ili kuwanufaisha wanafuzi hao, kuwaondolea usumbufu pamoja na kuwaondolea mazingira hatarishi” alisema Mwl. Gagula.
Pia aliongeza na kusema kuwa uwepo wa shule hii una manufaa makubwa sana kwa wakazi wa maeneo ya karibu. “Manufaa yatakayo patikana katika hili eneo ni pamoja na kuwapunguzia kero wazazi kwa ule usumbufu wa wanafunzi kuingia gharama kubwa kwenda umbali mrefu kupata elimu na manufaa ya pili ni kero ambazo wanafunzi walikua wanapata wakiwa njiani kama usafiri, kuchelewa kufika shuleni na nyumbani muda wa kurudi itakuwa imetatuliwa” aliongeza Mwl. Gagula.
Pia mkazi wa Mtaa wa Mbuyuni Mahungo, Kata ya Kizota, Joseph Wambura amemshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea shule karibu ili kuondoa changamoto ya watoto kwenda kusoma shule mbali na nyumbani. “Ninamshukuru, Mheshimiwa Rais wetu, mbunge na Diwani kwa ujenzi wa shule hii ya msingi kwasababu itaondoa changamoto ya watoto wetu kwenda umbali mrefu hapo awali walikua wanatembea takriban kilomita nane kuifuata shule. Mitaa ya Uhuru na Sokoine sasa tuna amani shule ipo karibu tutawajibika kuwakazania watoto wasome kwa bidii” alishukuru Wambura.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.