Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WILAYA ya Dodoma ilikusanya mapato ya shilingi 44,454,939,022 kupitia mifumo ya kieletroniki na kutekeleza miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Taarifa hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma, Sakina Mbugi alipokuwa akisoma risala ya utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Dodoma katika uwanja wa Shule ya Msingi Chamwino jijini hapa.
Ukusanyaji wa kodi na mapato kwa mfumo wa TEHAMA umeendelea kuimarika. “Mheshimiwa Rais; wilaya kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilifanikiwa kupata mashine za kielektroniki za kukusanyia mapato (POS) 304 na shilingi 44,454,939,022.82 zilikusanywa na kutumika kwenye miradi ya maendeleo” alisema Mbugi.
Kuhusu sekta ya biashara alisema malipo yote yanafanyika kupitia benki. “Mheshimiwa Rais; Wilaya ya Dodoma imefanikiwa kusajili wafanyabiashara kwenye mfumo wa serikali za mitaa wa ukusanyaji mapato na malipo yote ya ada za leseni za biashara yanafanyika benki. Mwaka 2022/2023 wilaya ilifanikiwa kutoa leseni za biashara 11,794 na leseni za vileo 1,034 zilizoingiza shilingi 1,979,525,035.90 sawa na asilimia 61.8 ya lengo” alisema Mbugi.
Akiongelea hali ya ulinzi na usalama kwa raia na mali zao alisema kuwa ni shwari na hakuna matukio makubwa ya uhalifu. “Wilaya ya Dodoma ina fursa nyingi zikiwemo viwanja vya makazi na biashara, eneo la viwanda Nala, miundombinu mizuri ya barabara za lami, ujenzi wa Reli ya mwendo kasi na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Msalato na vyuo vinavyotoa huduma za elimu” alisema Mbugi.
Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 unaongozwa na kaulimbiu isemayo “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa ustawi wa Viumbe Hai kwa Uchumi wa Taifa”
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.