Na. Coletha Charles, KIZOTA
WANANCHI wa Kata ya Kizota Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wanufaika na mradi wa ujenzi wa kituo cha afya kilichogharimu kiasi cha shilingi 500,000,000 kwa lengo la kusogeza huduma ya afya kwa wakazi wa kata hiyo.
Viongozi na wananchi wa kata hiyo wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha huduma ya afya inaboreka nchini kote hususan katika Kata ya Kizota.
Aidha Diwani wa Kata ya Kizota, Jamal Ngallya alisema kuwa kukamilika kwa kituo hicho kutaboresha kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa Kizota na maeneo jirani. “Kituo chetu kimejengwa kwa gharama kubwa sana, jumla ya shilingi 500,000,000 zimeletwa na serikali kukamilisha mradi huo ili wananchi wapate huduma nzuri na bora. Majengo yaliyojengwa katika kituo hiki ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje, jengo la mionzi, jengo la huduma ya mama na mtoto, jengo la maabara, kichomea taka, na yataongezwa majengo mengine kama wodi za wagonjwa pamoja na mochwari” alisema Ngallya.
Aliongeza kuwa Kituo cha Afya Kizota ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi vya afya jijini Dodoma kwa sasa, na kinatarajiwa kuwa cha tatu kwa ukubwa mara baada ya Makole na Ipagala. “Kupitia serikali ya awamu ya sita, tumepata kituo cha afya chenye majengo muhimu na ya kisasa. Hili ni jambo ambalo linaongeza hadhi ya kata yetu na linatoa fursa ya kupata huduma bora kwa karibu. Uboreshwaji wa huduma za msingi kwasasa unafika hadi katika ngazi ya kata” alisema Ngallya.
Nae, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Relini Kata ya Kizota, Lizi Edward, alisema kuwa ujio wa kituo hicho utaondoa adha kubwa kwa wakazi wa hapo, hasa mama wajawazito waliokuwa wakilazimika kwenda nje ya kata kupata huduma za uzazi na vipimo muhimu. “Kipekee sana tunaishukuru serikali kwa ajili ya kutupatia mradi huu wa kituo cha afya, kupitia kituo hiki watu wengi watakuja kupata huduma. Kwa sasa, wamama hawahitaji tena kuamka alfajiri au kulazimika kupanda usafiri wa mbali kutafuta huduma. Hii ni nafuu kubwa kwa familia nyingi” alisema Edward.
Kwa upande wake, Mkazi wa Mtaa wa Relini Kata ya Kizota, Yohana Richard, aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuwaletea mradi wa ujenzi wa kituo cha afya katika mtaa huo, na kusema kuwa ni neema kubwa kwa wakazi wa eneo hilo. “Kabla ya kituo hiki, tulikuwa tunahangaika sana. Tumeenda Makole, ‘General Hospital’, na wakati mwingine hadi Ntyuka kutafuta huduma za afya. Lakini sasa, ndani ya miaka minne tu ya uongozi wa Mama Samia, kituo hiki kimejengwa na tunajivunia kuona huduma hizi muhimu zinakuja karibu yetu na tunaimani tutaletewa madaktari bingwa ili tupate huduma zote muhimu” alisema Richard.
Hata hivyo, Mkazi wa Mtaa wa Relini, Cecilia Chundu, alisema kuwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kizota umeleta faida kubwa kwa wakazi wa eneo hilo, si tu kwa upande wa huduma za afya bali pia katika kuongeza ajira na kuinua hali ya kiuchumi ya wananchi, hasa vijana na wanawake. “Ninawashukuru sana viongozi wetu, akiwemo Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge wetu Anthony Mavunde, na Diwani wetu Jamal Ngallya kwa kutuletea mradi huu mkubwa. Vijana wetu walipata ajira wakati ujenzi unaanza, wakina mama wajasiriamali walinufaika. Na sasa bado tunatarajia kunufaika zaidi, hasa sisi kina mama tutakuwa na sehemu salama ya kujifungulia karibu na nyumbani. Awali tulikuwa tunahangaika sana, tulikuwa hatuna kituo cha afya kabisa hapa kata yetu, tulilazimika kwenda mbali kufuata huduma,” alisema Chundu.
Ujenzi wa kituo hicho si tu umetatua changamoto ya huduma za afya, bali pia umefungua milango kwa uwepo wa ajira kwa watoa huduma na kuimarisha uchumi wa ndani kupitia shughuli ndogo ndogo zinazozunguka kituo hicho. Kizota sasa inang’ara kwa maendeleo ya miundombinu na maisha ya kila siku ya wakazi yanaimarika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.