WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameagiza mkandarasi anayetekeleza mradi wa umeme vijijini, Awamu ya Tatu, mzunguko wa kwanza, mkoani Dodoma akatwe asilimia 10 ya malipo yake kutokana na kuchelewa kukamilisha kazi hiyo.
Waziri Kalemani ametoa agizo hilo leo, Agosti 12, 2020 baada ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chemba.
Akiwa amefuatana na Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga, Waziri Kalemani ameutaka uongozi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kukata kiasi hicho cha malipo ya mkandarasi Kampuni ya A2Z Infra Engineering Limited, kuanzia Juni 30, 2020 muda ambao alipaswa kukamilisha mradi.
Sambamba na hilo, Waziri pia amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vyote 66 vilivyobakia kabla ya Septemba 15 mwaka huu, huku akisisitiza kuwa, hakutakuwa na nyongeza ya muda wala msamaha.
"Asipomaliza ndani ya wakati huo, mchukulieni hatua za kisheria na kimkataba. Maeneo yatakayobaki fanyeni ninyi TANESCO kwa pesa hiyo".
Aidha, amemwagiza mkandarasi huyo kuongeza vibarua na magenge, ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati.
Vilevile, amemtaka kuondoa mara moja nguzo zote zilizorundikana chni na kuzisimika, kuvuta nyaya na kuwaunganishia umeme wananchi.
"Kiu ya wananchi ni kuona umeme unawaka katika nyumba zao. Hawapendezewi kuona nguzo zikiwa zimerundikana chini, nanyi mkipitapita pasipo kuwawashia umeme", amesisitiza Waziri.
Dkt. Kalemani ametoa wigo kwa wakandarasi wote nchini, wonaondelea na kutekeleza Miradi ya REA III, kuhakikisha wanakamilisha ifikapo Septemba 15, 2020
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya amemshukuru Waziri kwa kufuatilia utekelezaji wa mradi wa REA huku akiweka wazi kuwa hana imani na mkandarasi huyo kutokana na kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.
Mkuu huyo wa Wilaya ameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Waziri katika kumsimamia mkandarasi huyo anayefanya kazi katika Wilaya yake.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani akitoa maagizo mbele ya mkandarasi na timu ya Wilaya ya Chemba kuhusu utekelezaji wa mradi wa REA.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia) akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Chemba Simon Odunga (wa pili kushoto) akifafanua jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati kutembelea utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Wilayani Chemba mkoani Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.