HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) zimesaini hati ya makubaliano (MOU) ya upandaji, ustawishaji, na utunzaji wa miti na uhifadhi wa misitu iliyopo katika Jiji hilo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Kampeni ya Dodoma ya Kijani iliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Rais Mhe. Samia Saluhu Hassan kwa kupanda miti kwenye eneo la Mzakwe mwishoni mwa mwaka jana.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ambayo ni ya kwanza kufanywa na TFS Nchini ilifanyika jana katika Ofisi za Jiji, ambapo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi na Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo walisaini makubaliano hayo ambayo utekelezaji wake unaanza katika mwaka huu wa fedha.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo wakikabidhiana hati ya makubaliano.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali, Mkurugenzi Kunambi alisema Jiji linawakabidhi TFS hekta 150 za msitu katika eneo la Mahomanyika ili kustawisha miti na kulihudumia.
“Lakini pia kwa makubaliano haya, TFS watahifadhi maeneo yote ya vilima vilivyopo ndani ya Jiji la Dodoma na kustawisha misitu midogo katika maeneo ya makazi yaliyotengwa kwa ajili hiyo” alisema Kunambi.
Alisema hizi ni juhudi za kutekeleza kampeni ya Dodoma ya Kijani ambayo ina lengo la kulifanya Jiji la Dodoma na Mkoa mzima kustawisha miti ya kutosha ili kuhifadhi mazingira yatakayokuwa rafiki zaidi kwa maisha ya binadamu.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (kushoto) akifafanua jambo mbele ya Mtendaji Mkuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Professa Dos Santos Silayo kuhusu maeneo waliyokubalina kupanda na kustawisha miti, na kuhifadhi misitu iliyopo ndani ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kuikijanisha Dodoma.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TFS Profesa Silayo alisema kuwa tayari taasisi yake imetenga Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mpango huo alioutaja kuwa wa Kihistoria kwani haujawahi kufanyika katika Halmashauri yeyote Nchini, na kwamba utalipa hadhi kubwa Jiji la Dodoma kwenye Jumuiya ya Kimataifa.
“Makubaliano haya yataliweka Jiji la Dodoma katika ramani ya dunia katika kwenda na mahitaji ya maendeleo endelevu ya dunia kupitia mpango uendelevu wa Miji, lazima tujipange kukabiliana na ongezeko la watu na ukuaji wa Miji, Mpango huu utalifanya Jiji hili kwenda sambamba na kuweka uwiano sawia wa kiikolojia.” Alisema Profesa Silayo.
Makubaliano hayo yamesainiwa ikiwa ni takribani wiki mbili baada ya Jiji la Dodoma kuingia makubaliano na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) ya utunzaji wa mizunguko mitatu mikubwa ya barabara iliyopo Jijini humo, ambapo Mamlaka hiyo itahudumia bustani za maua na kuweka sanamu za Wanyama ikiwemo ya Tembo ili kupendezesha Mji na kutangaza vivutio vya kitalii vilivyopo Nchini.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.