Na. Mwandishi Maalum, KITETO
Mkoa wa Dodoma wapata hati safi katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 baada ya miradi yake 45 kukubaliwa na katika wilaya saba na halmasahuri nane za mkoa huo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule leo tarehe 7 Oktoba, 2023 wakati akikabidhi Mwenge wa Uhuru 2023 kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga katika uwanja wa Shule ya Msingi Dosidosi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto.
Senyamule akitoa taarifa ya hitimisho kwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 kwa Mkoa wa Dodoma, alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa kwa takribani kilometa 1893 na kupitia jumla ya miradi ya maendeleo 45.
Miradi 15 iliwekewa jiwe la msingi, miradi 19 ilizinduliwa na 11 ilitembelewa yote ikiwa na jumla ya thamani ya zaidi ya shilingi Billioni 16. Miradi hiyo ni pamoja na miradi ya sekta za elimu, afya na miradi ya utunzaji wa Mazingira aliongeza.
Aidha, alisema kuwa Mwenge wa Uhuru ulipita katika wilaya zote saba na Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma ambazo ni Bahi, Chemba, Kondoa DC, Kondoa Mji, Dodoma Jiji, Chamwino, Mpwapwa na kumaliza mbio zake kwenye Wilaya ya Kongwa.
"Dada yangu Queen Sendiga na viongozi wote mliokusanyika hapa nitumie fursa hii kuwatangazia na kuwajulisha kwamba, miradi yote 45 katika Mkoa wa Dodoma ilipita salama bila kukataliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2023. Hivyo, niwapongeze sana wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu 2023 kwa kazi hii iliyotukuka mlioifanya Dodoma" alieleza Senyamule.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, aliahidi kutekeleza maelekezo kwa sehemu zote ambazo viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru walishauri kufanyiwa marekebisho na mkoa utahakikisha maeneo hayo yanaboreshwa.
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga wakati akipokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisema kuwa Mwenge wa Uhuru utakapo kuwa mkoani kwake utatembelea miradi ipatayo 57 yenye thamani ya jumla ya shilingi Billioni 13.2, utaweka jiwe la msingi, utazindua na kukagua miradi mbalimbali.
Nae, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Taifa, Abdalla Shaib Kaim aliupongeza Mkoa wa Dodoma kwa kupata hati safi katika miradi yote iliyokaguliwa na Mwenge wa Uhuru huku akifurahishwa na ushirikiano uliooneshwa na viongozi katika kipindi chote Mwenge wa Uhuru ulipokua ndani ya Mkoa huo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.