UONGOZI wa Mkoa wa Dodoma umeridhishwa na muendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya kijanisha Dodoma unaofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo kwa lengo la kulinda na kutunza mazingira.
Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Natalius Linuma alipokuwa akitoa shukrani kwa washiriki wa zoezi la upandaji miti kwa timu “B” lililofanyika katika shule ya msingi Ipala jijini hapa.
Linuma ambaye pia ni Katibu Tawala msaidizi, anayesimamia menejimenti ya Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, alisema kuwa mheshimiwa mkuu wa mkoa aliagiza kila mtumishi apande miti angalau 10 kila siku ya Jumamosi. Aidha, aliipongeza halmashauri ya jiji hilo kwa muitikio huu ambao ni utekelezaji wa agizo la mheshimiwa Mkuu wa Mkoa. “Sasa wito wangu kwenu ni kuitunza miti hii na kuhakikisha inakuwa. Ili kampeni hii itoe mafanikio makubwa haraka lazima tuongeze kasi ya upandaji miti na kuitunza” alisema Linuma.
Mwakilishi huyo, aliupongeza uongozi wa kata ya Ipala kwa kuwa mstari wa mbele katika upandaji miti. “Hapa Kata ya Ipala mmejitahidi sana kupanda miti, naona idadi ya miti iliyopandwa ni kubwa na inaendelea vizuri. Natamani Kata zote ziige mfano wa kata hii” alisema Linuma.
Awali mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo (pichani juu) alisema kuwa jumla ya miti 1,500 ilipandwa katika zoezi la upandaji miti katika Kata ya Ipala.
Mwalimu Mabeyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma alisema kuwa katika zoezi hilo, limehusisha upandaji wa miti ya matunda. “Wote tumeshuhudia katika zoezi hili tumepanda pamoja na miti mingine, miti ya matunda. Lengo ni kuboresha lishe ya wanafunzi. Wanafunzi wanapokuwa na afya njema inawawezesha kupata maarifa na ujuzi kwa uhakika. Hivyo, lishe bora itawafanya wanafunzi kuwa huru dhidi ya magonjwa na kutumia muda wao vizuri katika masomo” alisema Mwalimu Mabeyo.
Matunda pia ni sehemu ya chakula, hivyo yatakapokuwa na kukomaa yatawavutia wanafunzi kuyatumia kama matunda na chakula. Matumaini ya halmashauri ni kwamba, matunda haya yatasaidia kuondoa utoro kwa wanafunzi, aliongeza.
Nae mratibu wa kampeni ya kijanisha Dodoma, katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro alisema kuwa halmashauri ilizigawanya timu mbili za watumishi wa halmashauri ili kuharakisha zoezi la upandaji miti. Alisema kuwa timu “A” iliongozwa na Mkurugenzi wa Jiji na timu “B” iliongozwa na Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi.
Zoezi la upandaji miti katika shule ya msingi Ipala iliyopo Kata ya Ipala lilishirikisha watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Jiji, Mthibiti ubora wa wilaya, Tume ya Utumishi wa Walimu, Wakala wa Misitu Tanzania, Kata ya Ipala na wananchi kwa ujumla.
Mthibiti Ubora wa Elimu Wilaya ya Dodoma Mjini, Mwalimu Lucy Mbolu akisiriki kupanda mti wake wa 11 wa mpapai katika shule ya msingi Ipala iliyopo jijini Dodoma katika utekelezaji wa kampeni ya Kijanisha Dodoma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.