Na. Aisha Ibrahim, MADUKANI
MIKOPO ya asilimia 10 isiyo na riba kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma imekuwa na tija kwa vikundi vya wajasiriamali na kuwasaidia kukuza kipato na kuinua uchumi katika Kata ya Madukani.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Maendeleo ya Jamii, Kata ya Madukani, Asha Hussein alipokuwa akiongelea mikopo hiyo na umuhimu wake kwa wananchi wa kata ya madukani.
Alisema kuwa katika kata hiyo kuna jumla ya vikundi 14 vilivyopatiwa mkopo wa kiasi cha shilingi milioni 273, ambapo wanawake ni vikundi saba na walipata kiasi cha shilingi milioni 160 na vijana ni vikundi saba waliopokea kiasi cha shilingi milioni 113.
Alisema kuwa kutokana na mikopo hiyo wanufaika wameweza kuanzisha shughuli mbalimbali zinazowaingizia kipato na kuweza kujiinua kiuchumi. “Asilimia kubwa wana vikundi na wameanzisha shughuli zao za kuwaingizia kipato. Mfano; kuna baadhi yao wanauza nguo, kuna vijana wamefungua duka la madawa, ufundi wa simu na baadhi ya wakina mama wanajishughulisha na ushonaji na wamefungua saluni za kike, mbali zaidi wapo wengine wanafanya shughuli za ufugaji nje ya kata hii” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi cha Vijana cha Edame, William Frank, kutoka Kata ya Madukani, alisema kikundi hicho kinajishughulisha na ufundi wa kompyuta, funguo na simu, na kupitia mkopo wa asilimia 10 wameweza kununua vifaa kwaajili ya kuendeshea shughuli zao na kufanikiwa kuajiri baadhi ya vijana wenye ujuzi katika fani hiyo. “Kupitia mkopo wa asilimia 10 kwa vijana, tumeweza kununua vifaa vya kuendeshea shughuli zetu, mbali zaidi tumeajiri mpaka vijana wenye taaluma ya ufundi na wanafanya kazi vizuri” alisema Frank.
Vilevile, aliwaasa vijana kuwa na hali ya uthubutu hata kama hawana mitaji ya kujiajiri waweze kujitoa kufuata taratibu za kupata mikopo hiyo itakayowasaidia kuendesha maisha yao kwasababu haina riba. “Niwaase vijana wenzangu hata kama hawana mtaji wa kuanzisha shughuli yoyote twende tukaombe mikopo hiyo isiyo na riba, hii itasaidia tuweze kujiajiri wenyewe na kuweza kuendesha maisha yetu ya kila siku” alisema Frank.
Nae, mnufaika wa mikopo hiyo, Elizabeth Sebastian, kutoka Kikundi cha Wanawake cha Amani, alifafanua kuwa kikundi hicho chenye jumla ya wanachama watano, walifanikiwa kupata mkopo wa kiasi cha shilingi 10,000,000 uliowasaidia kufanya maendeleo na kujikwamua kiuchumi. “Mkopo huu tulioupata tulifanikiwa kuanzisha mradi wa asali na tulikuwa na mizinga ya nyuki, lakini kutokana na changamoto tukaamua kufungua duka la nguo na kupitia mkopo tulioupata mara ya pili duka letu limekuwa kubwa na tumeweza kujikwamua kiuchumi. Kupitia mikopo hii tunaweza kutunza familia zetu na kutimiza majukumu mbalimbali ya hapa na pale. Pia tunapambana kuepuka kuwa tegemezi katika jamii kwasababu maendeleo katika jamii yanakuja kutokana na juhudi za kupambana” alisema Sebastian.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.