MKURUGENZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi ameahidi kuwakatia Bima ya Afya wafanyakazi 133 wanaosafisha mitaa na barabara zote za Mji wa Dodoma ili wawe na uhakika wa matibabu wao na familia zao.
Alitoa ahadi hiyo jana alipofanya mkutano na wafanyakazi hao katika viwanja vya Nyerere katikati ya Mji wa Dodoma ambapo pia aliwapatia fedha taslimu Shilingi 10,000 na mche mmoja wa sabuni kila mmoja kama zawadi kuelekea mwisho wa mwaka 2017.
Mkurugenzi Kunambi alisema kuwa, yeye kwa niaba ya Uongozi wa Manispaa ametoa zawadi na ahadi ya kuwakatia Bima ya matibabu baada ya kufurahishwa na uchapa kazi wao unaopelekea mitaa na barabara za Mji kuwa safi na kupendeza muda wote.
“Hiki tunachowapa leo hakina thamani yeyote kwa kazi kubwa mnayoifanya, bali ni kuonesha kuguswa kwetu tu kama Manispaa…ninyi ni kundi maalum na ni wafanyakazi muhimu sana” alisema Kunambi akizungumza na watumishi hao.
“Nimefurahi kukutana na kuzungumza na ninyi kipindi hiki cha mwisho wa mwaka…nawaahidi mapema mwakani Manispaa itawakatika Bima za Afya wote itakayomwawezesha kila mmoja kutibiwa yeye na wategemezi wake watatu” alifafanua.
Kwa upande wao, wafanyakazi hao ambao wengi wao ni akina Mama walimshukuru Mkurugenzi huyo kwa niaba ya Manispaa kwa kuwajali licha ya kuwa wao ni watumishi wa kada ya chini na wanaofanya kazi kwa mkataba isiyo ya kudumu.
“Tumefurahi sana leo Mkurugenzi wetu umekuja kuongea na sisi na kutupa zawadi na fedha tena katika kipindi cha Sikukuu za mwisho wa mwaka...umetujali sana na sisi tunakuombea kwa Mugu”… alisema mmoja ya akia mama hao akimshukuru Mkurugenzi wa Manispaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.