Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, amekabidhi hati za viwanja kwa wananchi 144 wa Kata ya Tambukareli ambao maeneo yao yalikuwa yametwaliwa na Serikali.
Kunambi amekabidhi hati hizo kwa wananchi hao ambao wamekuwa wakihangaika kwa miaka minne na kueleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma itahakikisha kila Mwananchi anapata haki yake kama ambavyo Rais Dk John Magufuli amekua akisisitiza kuwatumikia wanyonge.
“Leo hii hapa kuna zoezi la kutoa viwanja kwa wananchi ambao ni wahanga wa maeneo yao ambao awali inadaiwa yalitwaliwa na iliyokua Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kuwaacha ndugu zetu hawa wakiwa hawana maeneo".
“Kwa muda mrefu kumekua na malalamiko ya wananchi na sisi kama Jiji tulifanya tathmini ya jumla na kuona ndugu zetu hawa wana haki ya kulipwa fidia ya maeneo yao na hivyo leo tumemaliza kero yao ya muda mrefu kwa kuwagawia viwanja bure na watakacholipia wao ni zile tozo za kawaida za kikatiba,” amesema Kunambi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo, Mheshimiwa Juma Mazengo, amemshukuru Mkurugenzi Kunambi kwa jinsi alivyolivalia njuga suala lao na kuweza kumaliza kero ya wananchi wake ambao wameteseka kwa miaka minne.
“Nimshukuru Rais Magufuli, kweli tumeona jinsi gani anatetea wanyonge. Hii inaonesha jinsi gani anaziishi ahadi zake alizowaahidi wananchi wakati wa kampeni, tunayo furaha sana na hakika tumeona heshima tuliyopewa na Serikali yetu,” amesema Mazengo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.