Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amekabidhi vitambulisho kwa Wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama Machinga wanaofanya shughuli zao katika "Soko la jioni" ili waweze kufahamiana wakati wa biashara zao na hata kusaidia kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama.
Wafanyabiashara ndogo ndogo wapatao 140 wanaofanya shughuli zao pembeni ya eneo la Viwanja vya Nyerere wamekabidhiwa vitambulisho hivyo na Mkurugenzi huyo katika hafla fupi iliyofanywa katika viwanja hivyo mchana wa leo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Kunambi amewaasa wafanyabiashara hao kuwa na utamaduni wa kutunza akiba ili kukuza mitaji yao huku akiwaahidi kuwaboreshea mazingira ya kazi zao na kwamba hakuna kiongozi atakayewaondoa katika maeneo hayo mpaka watakapopatiwa maeneo mbadala na rafiki kwa biashara zao.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Magufuli ni rafiki wa Machinga na ameshatoa maelekezo na nyinyi ni mashahidi…nawaahidi kusimamia maagizo ya Rais ya kuhakikisha wananchi wanyonge hawanyanyasiki ndani ya Nchi yao” alisema Kunambi.
Aliwataka wafanyabiashara kujiandaa kutumia fursa za ujenzi wa stendi mpya na ya kisasa na soko kubwa kwa ajili ya wafanyabiashara vitakavyojengwa katika Kata ya Nzuguni ili waweze kukua kibiashara.
“Tunaanza ujenzi wa stendi kubwa ya kisasa na ya mfano Afrika Mashariki na Kati katika eneo la Nzuguni Mwezi Machi 2018…ujenzi utakamilika baada ya miezi 24 na utaenda sambamba na ujenzi wa soko kubwa la kisasa kwahiyo jiandaeni kutumia hizo fursa” alisisitiza.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.