Na. Valeria Adam, Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, ametembelea miradi ya serikali iliyopo Kata ya Mtumba na kusisitiza elimu kuwa agenda ya kudumu.
Akizungumza na walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtumba alitoa wito kwa jamii kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kitaaluma, ufundishaji na ujifunzaji ili kuhakikisha majengo mazuri yaliyojengwa yanaakisi ubora wa elimu.
Alisema kuwa ni muhimu katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu bora na yenye tija, na kwamba walimu wana nafasi kubwa katika kufanikisha hilo. “Nisisitize agenda hii ya elimu iwe ni ya kudumu, fuatilieni kwa karibu maendeleo ya kitaaluma, ufundishaji ili kusudi majengo haya mazuri tuliyojengewa yaakisi katika ubora wa elimu” alisema Alhaj Shekimweri.
Aidha, aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwataka waendelee kuwafundisha watoto kwa upendo na kwa kuwajali ili kuwasaidia watoto kujifunza vizuri bila kuhofia chochote. “Walimu muwafundishe watoto kwa upendo, muwaelekeze kwa kuwajali, muwasimamie katika maendeleo yao ya kitaaluma. Pia muwashirikishe wazazi ili waweze kujua tabia na mienendo ya watoto wao katika taaluma” alisisitiza Alhaj Shekimweri.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mtumba, Mwl. Kepha Kitutu alisema kuwa mradi wa ujenzi wa vyumba saba vya madarasa umesaidia katika kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa. Alisema kuwa mradi umekamilika kwa asilimia 100 bila kuwa na deni lolote kutoka kwa wazabuni au mafundi ujenzi wa shule hiyo.
“Shule hii ina jumla ya wanafunzi 1,438 (wavulana 699 na wasichana 739), kabla ya mradi ilikuwa na vyumba 31 vya madarasa pekee. Hali ya madarasa ilikuwa mbaya sana, na baadhi yalikuwa chakavu na kuhatarisha usalama wa wanafunzi na walimu. Hivyo, kusababisha mrundikano mkubwa wa wanafunzi.
“Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na madawati 30 kutoka mradi wa EP4R umekamilika kwa asilimia 100. Ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa kutoka mapato ya ndani umekamilika kwa asilimia 100. Ujenzi na utekelezaji wa mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 bila ya kubaki na deni lolote kutoka kwa wazabuni au mafundi ujenzi” alihitimisha Mwl. Kitutu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.