MKUU wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri amewataka Wananchi wa Kata ya Viwandani kuchukua kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto ikiwa ni pamoja na kumiliki na kujua kutumia vizimia moto (Fire Extinguishers).
Mhe. Shekimweri ameyasema hayo alipotembelea eneo kulipotokea moto usiku wa kuamkia leo (tarehe 18 Julai, 2021) ba kuteketeza nyumba moja nayomilikiwa na Abduelly Mstahafu na sehemu ya kulala wageni ya ‘Holiday Guest House’. Mkuu wa Wilaya aliongozana na Diwani wa Kata ya Viwandani Mhe. Jaffary Mwanyemba na Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Dodoma Deogratias Inano.
Aidha, Mheshimiwa Shekimweri aliwataka wananchi kujitahidi kukatia bima ya moto nyumba zao ili inapotokea hasara kama hiyo Bima waweze kuwalipa. Akihitimisha nasaha zake, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliwaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UVIKO-19 vinavyosababisha ugonjwa wa Korona kwa kuvaa barakoa wanapokuwa katika mikusanyiko, kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu na kunawa kwa sabuni na maji safi tiririka.”
Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (M) Dodoma kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi umebaini chanzo cha moto ulioteketeza nyumba hiyo iliyopo mtaa wa Baruti kata ya Viwandani jijini Dodoma kuwa ni Sigara
Akizungumza baada ya Uchunguzi Mkaguzi Msaidizi wa Zimamoto na Uokoaji (M) Dodoma Deogratias Inano amesema, chanzo cha moto huo ni sigara iliyokuwa ikivutwa na mtoto wa mwenye nyumba aliyejulikana kwa jina la Mohamed Omari (35) ambaye ana matatizo ya akili.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni dada yake na Mohamed amesema, alimuona kaka yake akitokea chumbani na baada ya muda mfupi chumba kilianza kuwaka moto.
Alisema kuwa kaka yake huyo huwa ana tabia ya kuvutia sigara ndani na mara ya mwisho alimuona akiingia ndani na sigara kama ilivyo kawaida yake na alipotoka ndani ndipo alipoona dalili ya moto katika chumba kile
“Nilimuona kaka Muddy akivuta sigara na kuingia nayo ndani, baada ya muda mfupi alitoka na ndipo tulipoona dalili ya moto katika chumba kile. Nilipoenda kuangalia nilikuta godoro limeshika moto na ndipo moto ulipotuzidi na kuteketeza nyumba” Alisema dada huyo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Jabir Shekimweri (katikati) akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Viwandani kulipotokea moto na kuteketeza nyumba. Kulia ni Mheshimiwa Jaffary Mwanyemba, Diwani wa Kata ya Viwandani ilipo nyumba hiyo, na Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma Deogratias Inano (kushoto).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.