Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuwapanga upya Wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama Wamachinga, bila kutumia nguvu ili wafanye biashara zao kwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Mhe. Rais Samia ametoa agizo hilo leo mara baada ya kuwaapisha viongozi aliowateua jana tarehe 12 Septemba, 2021 katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.
Mhe. Rais amesema Serikali ilitoa fursa kubwa kwa Wamachinga kufanya biashara na kujipatia kipato kwa uhuru lakini wametumia fursa hiyo vibaya na kufanya biashara kiholela ambapo baadhi yao hupanga bidhaa nje ya maduka na kuwazuia wenye maduka kufanya biashara, kitendo ambacho kinaikosesha Serikali kodi toka kwa wafanyabiashara hao.
Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka viongozi aliowaapisha na walio katika nafasi mbalimbali za uongozi kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa kuwa mabadiliko aliyofanya katika Baraza la Mawaziri ni ya kawaida lakini ni endelevu.
Mhe. Rais Samia amewataka watendaji Serikalini kuendesha shughuli zao kwa vitendo ili kuwaletea wananchi maendeleo na si kwa maneno makali ambayo hayana tija kwa maendeleo ya wananchi.
Awali, Mhe. Rais Samia amemuapisha Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. January Yusuf Makamba, kuwa Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Dkt. Stergomena Lawrence Tax, kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya Siasa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.