WANANCHI wilayani Dodoma mjini wameshauriwa kutouza ardhi kiholela badala yake kupata msaada wa kisheria kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Mwalimu Josephat Maganga alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Mtumba jijini Dodoma jana katika ziara yake ya kujitambulisha, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mwalimu Maganga alisema “ndugu zangu wapendwa wana Mtumba pamoja na mitaa yetu yote minne, Vikonje ‘A’, Vikonje ‘B’, Majengo na Mtumba, hii ardhi tunayoiona kama wanavyosema, zamani haikuwa na thamani. Lakini tumekuja kugundua kwamba ina thamani kubwa. Wananchi tunaongezeka, tunakuwa wengi lakini ardhi ipo hivyo hivyo. Hii ardhi ni kitu cha thamani, ina thamani kiuchumi, tunalima kwenye ardhi hii tunapata chakula, tunajenga kwenye ardhi hii nyumba zetu na tunaishi, tumezaliwa kwenye ardhi hii na inawezekana, na ni kweli kabisa kwamba hata kufa tutazikwa kwenye ardhi hii”.
Alisema kuwa ardhi ni kitu cha thamani na yanapofanyika maamuzi ya ardhi wanaoyafanya wahakikishe wanafanya maamuzi sahihi. Aidha, aliwataka Wenyeviti wa Mitaa na watendaji kuwa makini na uuzaji ardhi. “Ndugu zangu naomba tuwe makini na uuzaji holela wa ardhi, tuwe makini sana. Hata kama mwananchi wa kawaida anataka kuuza eneo lake, sheria zinaturuhusu kuhoji, kwa sababu anaweza akauza ardhi hapa, mkashitukia anakuja mtu anatengeneza mambo ya baruti hapa, ukimuuliza anasema anapasua miamba hapa halafu anasababisha matatizo. Tutahitaji kujua huyo mtu ni nani? anatoka wapi na kwanini aje anunue ardhi kubwa hapa. Kuna wakati mwingine wanakuja watu wataalam kuwazidi hata nyie wenyewe. Niwaombe kabla ya kufanya maamuzi shirikisheni Halmashauri ya Jiji, lazima itatoa msaada wa kisheria” alisema Mwalimu Maganga.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga shilingi milioni 210 kwa ajili ya kulipa fidia wananchi waliotwaliwa maneo yao. “Nafurahi kuona hawa wananchi 34 wanapata fidia zao shilingi milioni 210. Niipongeze Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga fedha hizo ambazo nimetaarifiwa zitalipwa mwezi huu” alisema Mwalimu Maganga.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, Mwalimu Josephat Maganga akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi wa Kata ya Mtumba jijini Dodoma jana (16/08/2020) katika ziara yake ya kujitambulisha, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.