Na. Valeria Adam, Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora na kufuatiliwa kwa karibu ili wafaulu.
Aliyazungumza hayo katika ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa madarasa nane na matundu 10 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mtumba jijini Dodoma.
Alhaj Shekimweri alisisitiza umuhimu wa kuwapeleka watoto shule na kusimamia maendeleo yao ili kuwawezesha kufaulu kwa kiwango cha juu. “Tupeleke watoto wetu shule na sio tu kuwapeleka shule, tuwasimamie pia wafaulu. Kama dhamira ni kufanya watoto wetu wasome hapahapa, ni vema waje na watoto wa nje wajichanganye na watoto wetu ili kufundishana tamaduni mbalimbali na tutajenga watanzania wenye umoja” alisema Alhaj Shekimweri.
Mkuu wa Wilaya alisisitiza pia umuhimu wa kuweka uzio kwenye shule hiyo ili kuhakikisha usalama na kudhibiti uvamizi. Aliongeza kuwa, ingawa ujenzi wa uzio wa matofali ni chaguo zuri, mbinu rahisi kama matumizi ya miti au michongoma inaweza kuwa hatua ya awali ya kufanikisha lengo hilo. “Nihimize kuhusu suala la kuanza kufikiria uzio na kwenye uzio viongozi msijibane sana kwenye mawazo ya kujenga uzio wa matofali japokuwa ni kitu kizuri, lakini kwa kuanzia tutaweka hata miti au michongoma” aliongeza Alhaj Shekimweri.
Aidha, alitoa wito kwa taasisi za umma kuhakikisha maeneo yao yamepimwa na kuwa na hati ili kuepusha uvamizi na migogoro ya ardhi. Alieleza kuwa na mipaka rasmi kutasaidia kudhibiti changamoto hizo na kuweka mazingira salama kwa shule na taasisi nyingine. “Niendelee kusisitiza umuhimu wa taasisi za umma kuwa zimepimwa na zina hati, itasaidia sana uvamizi kutokuendelea kwa sababu kutakuwa kumepimwa kwa kila eneo na kuna mipaka. Kwa hiyo, niombe Afisa Elimu usimamie hili kwa niaba ya mkurugenzi kuhakikisha kwamba shule yetu na shule nyingine zinakuwa zimepimwa” alisisitiza Alhaj Shekimweri.
Nae Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtumba, Mwl. Stephen Mwenda alisema kuwa katika kukamilika kwa mradi huo kulikuwa na changamoto ambazo zilijitokeza ikiwemo kubadilika kwa bei za vifaa vya ujenzi. Changamoto nyingine ni ucheleweshaji wa upatikanaji wa saruji na upatikanaji wa maji kwa wakati wa ujenzi. “Kubadilika kwa bei za vifaa vya ujenzi katika masoko, ucheleweshaji wa upatikanaji wa saruji kulingana na maelekezo ya kitengo cha Manunuzi. Vilevile, upatikanaji wa maji umekuwa changamoto kutokana na kuwa na chanzo kimoja tu cha maji (Mfuko wa Maji Mtumba-RUWASA)” alisema Mwl. Mwenda.
Licha ya changamoto hizo Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtumba aliainisha mafanikio makubwa yanayotarajiwa kutokana na mradi huo. “Mradi huu umetoa ajira kwa wananchi wa Jiji la Dodoma na kuwapa mafunzo ya kazi, pamoja na kuwezesha mazingira mazuri ya kujifunza kwa wanafunzi. Pia, shule hii itakuwa ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha wanafunzi wa kidato cha tano kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania” alisema Mwl. Mwenda.
Jumuiya ya Shule ya Sekondari Mtumba ilitoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zinazosaidia kuboresha mazingira ya kujifunza kwa watanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.