Na. Faraja Mbise. DODOMA
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda amewataka wanawake wafanyabiashara wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuachana na mikopo ya Kausha damu na mwendokasi inayowanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake kutokana na muda wa marejesho na kiwango cha riba kuwa kikubwa na hivyo kushindwa kujikwamua kiuchumi na kuwaongezea umasikini zaidi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akizungumza katika Uzinduzi wa Umoja wa Wanawake Wafanyabiashara Masoko yote katika Jiji la Dodoma (UWAWAMA), uliofanyika Cathedral Social Hall, tarehe 01 Novemba, 2024.
Chatanda aliwataka wanawake wafanyabiashara kuachana na mikopo ya kausha damu na kujiunga na vikundi ili kupata mikopo ambayo inatolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma. "Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluh Hassan imerejesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa utaratibu ulioboreshwa zaidi ikiwemo kutumia benki kwa halmashauri kumi za majaribio zikiwemo za Dodoma" alisema Chatanda.
Kuhusu mikopo ya kausha damu, aliwataka wafanyabiashara kuachana nayo kwasababu inarudisha uchumi wa nchi nyuma na mwanamke anashindwa kujikwamua kiuchumi kutokana na masharti magumu ya riba na muda uliowekwa katika mikopo hiyo. "Sasa nawahimiza kuchangamkia fursa ya mkopo usio na riba tuliyopewa na serikali na kuondokana na mikopo ya kausha damu, ujinga na mwendokasi inayowanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake kutokana na utaratibu wa mikopo hiyo ukiwemo muda wa marejesho na kiwango kikubwa cha riba kuwa kikubwa hivyo badala ya kujikwamua kiuchumi inaongeza umaskini zaidi" alisisitiza Chatanda.
Katika kuhamasisha wanawake walengwa wa mikopo, alitoa rai kwa viongozi wanawake kuhamasisha wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na serikali. "Natoa wito kwa viongozi wanawake kuhamasisha walengwa wa mikopo hii wachangamkie fursa ya mikopo inayotolewa na serikali yao" alisisitiza Chatanda.
Aidha, aliwashukuru wanawake wa nchi nzima kuitikia wito wa kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024.
"Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inaonesha wanawake walioandikishwa ni asilimia 51.29 na asilimia 48.71 ni wanaume. Asanteni sana wanawake kwa kuiheshimisha serikali, kiongozi wetu mkuu wa nchi pamoja na mimi mwenyekiti wenu ambaye wakati wa ziara zangu zote nimekuwa nikiwasihi wanawake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha" alieleza Chatanda.
Uzinduzi wa umoja wa wanawake wafanyabiashara masoko yote katika Jiji la Dodoma ulihudhuriwa na wanawake wa masoko mbalimbali kama Soko kuu la Job Ndugai, Sabasaba, Majengo, Machinga na Bonanza. Pia na vikundi mbalimbali kama Wanawake na Samia, wanawake na Nyerere, Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Dodoma Jiji (JUWAKIDO).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.