Na. Josephine Kayugwa, DODOMA
Makisio ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya shilingi 128,278,555,369 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri ni bajeti ya wafanyakazi kwa sababu imezingatia maslahi ya wafanyakazi.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alipokuwa akitoa maoni juu ya makisio ya Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/2024 baada ya kupitishwa na mkutano maalum wa Baraza la Madiwani.
Gondwe alisema “bajeti hii ni bajeti ya wafanyakazi. Ni bajeti ya wafanyakazi kwa sababu nikirejea kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Jiji la Dodoma kilichofanyika tarehe 9 Januari, 2023 kwa mara ya kwanza wafanyakazi waliipongeza bajeti ya halmashauri na kusema imezingatia maslahi ya wafanyakazi. Baraza lilipongeza kwa kulipa madai mbalimbali ya walimu kwa maana ya likizo, wastaafu, uhamisho pamoja na waliofariki.
Nami niungane nao kumpongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru pamoja na timu yake ya Menejimenti kwa kujipanga katika bajeti hii. Hawa ni watu makini, kwa tafsiri nyepesi ya watu makini ni watu wanaowajali wanaowaongoza na kuwasimamia”.
Ufanisi wa makisio ya bajeti hii ulianzia kwenye maelekezo ya Mkurugenzi wa Jiji kwa wakuu wa divisheni na vitengo kuwataka wawashirikishe wafanyakazi walio chini yao katika uandaaji wa bajeti. “Wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi nilikuwa nikiona nuru katika nyuso za wafanyakazi, nilikuwa nikiona matumaini katika nyuso za wafanyakazi maana yake waliyakubali mapendekezo ya makisio ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma” alisema Gondwe.
Akiongelea maeneo yaliyopewa umuhimu zaidi aliyataja kuwa ni stahiki za watumishi na uhamisho. Maeneo mengine ni matibabu, vifaa vya ofisi, mazingira bora ya kufanyia kazi, likizo, posho ya kujikimu kwa watumishi wapya. Mengine ni kodi kwa watumishi katika mifuko ya hifadhi ya jamii, na ulipaji wa madeni mbalimbali.
“Nichukue nafasi hii kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa umahiri katika makusanyo ya mapato ya ndani. Makisio ya mwaka 2021/2022 yalikuwa shilingi 43,616,465,099, mapato hadi Juni, 2022 yalikuwa shilingi 44,379,552,980 sawa na 102% haya ni mafanikio makubwa” alisema Gondwe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.