Na. Calvin Gwabara, DODOMA
Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imekabidhi Juzuu za toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2023 kwa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na kupongeza mchango mkubwa uliotolewa na Ofisi hiyo kupitia watumishi wake kwenye utekelezaji wa zoezi la Urekebu.
“Wakati tunaanza zoezi hili Ofisi yetu ilikuwa na changamoto kubwa ya uhaba wa watumishi hasa Mawakili wa kufanya kazi hii lakini tulikuwa tukibisha hodi kwenye Ofisi yako kuomba Mawakili kuja kushirikiana nasi katika kutekeleza zoezi hili, na hakika walitusaidia sana hadi tumekamilisha” alieleza Katuga.
Aliongeza “Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kutambua mchango wenu imeona ni muhimu na Ofisi yako pia ipate nakala hizi ingawa tunatambua kuwa tumeleta chache kutokana na gharama lakini ziwasaidie kwa kuanzia na kuwa kama kumbukumbu kwenu, lakini mnaweza kupata nakala laini zote kupitia mfumo wa OAG MIS library” alieleza Katuga.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Divisheni ya Urekebu, Tafiti na Mafunzo ameongeza kuwa pamoja na nakala hizo tano pia wameipatia Ofisi hiyo tuzo maalumu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa lengo la kutambua mchango wa Ofisi ya Taifa ya Mashitaka katika zoezi hilo la Urekebu wa Sheria.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Ofisi yake Mkurugenzi wa Mashitaka, Sylvester Mwakitalu alipongeza kazi kubwa iliyofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) na kushukuru kwa kuwapatia nakala hizo za kuanzia kwaajili ya Ofisi yake maana wangeenda kununua dukani ingekuwa gharama kubwa.
“Ofisi yetu tunatumia Sheria hizi kila siku maana tunatoa huduma za mashitaka kwenye mahakama zote nchini hasa hasa Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi ndiko tunaenda huko kila siku, lakini pia Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa. Kwahiyo, hizi Sheria ni nyenzo muhimu sana kwetu” alieleza Mwakitalu.
Aliongeza “nakala hizi tulizozipata tutazisambaza kwa Mawakili wetu kwanza, alafu sisi tutaendela kusubiria kupata zingine kwa utaratibu maalumu lakini pia kwa kutumia zle ambazo zinazopatikana kwenye mfumo kwa nakala tepe”.
Toleo la Urekebu wa Sheria la Mwaka 2023 lilizinduliwa na kwa mujibu wa Sheria na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan mwezi Aprili, Mwaka huu na kutangaza kuanza kutumika tarehe 1/07/2025 na hivyo kufuta Toleo la Sheria la Mwaka 2002.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.