Na. Noel Rukanuga, DODOMA
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kutumia kalamu zao kwa uadilifu, kwa kuzingatia maadili ya taaluma na kuhakikisha wanahabarisha umma kwa namna inayolinda amani na usalama wa taifa.
Akizungumza wakati akifunga kikao kazi cha siku mbili kati ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wahariri wa vyombo vya habari, kilichofanyika leo Septemba 12, 2025 katika Ukumbi wa Mkemia Mkuu wa Serikali, jijini Dodoma, Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Kisheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Ipyana Mlilo, amesema kuwa sekta ya habari ni mhimili muhimu katika maendeleo ya taifa, hivyo kikao kazi hicho kimetoa nafasi ya kuimarisha ushirikiano baina ya wahariri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, ili kuendelea kutoa elimu ya kisheria kwa jamii kwa weledi.
“Kikao hiki kimekuwa na manufaa makubwa katika kuhakikisha jamii inapata uelewa mpana kuhusu masuala ya kisheria. Tumejadiliana mambo mengi muhimu ambayo yatashughulikiwa kwa lengo la kuelimisha na kulinda maslahi ya umma,” alisema Mlilo.
Alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili ya taaluma na kuhakikisha wanachangia katika ustawi na usalama wa taifa.
Akiwasilisha taarifa ya majukumu ya Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), Rais wa Chama hicho Bavoo Junus, amesema kuwa kuwa TPBA ni Chama muhimu katika kusimamia, kulinda na kutetea maslahi ya Serikali na rasilimali zake.
Alibainisha kuwa TPBA ni chama cha kitaaluma kinachowaunganisha wanasheria wote wanaohudumu katika taasisi za umma ikiwemo Wizara, Halmashauri, Wakala, na Mashirika ya umma pamoja na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa.
“Kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, TPBA imefanikiwa kueneza elimu ya sheria kwa wananchi wote Tanzania Bara na Zanzibar,” alisema Junus.
Aliongeza kuwa TPBA limeanzisha jukwaa la mawakili wa serikali kwa ajili ya kubadilishana uzoefu kitaaluma, kujadili changamoto, na kuweka mikakati ya pamoja ya kutetea maslahi ya Serikali.
Pia alieleza kuwa chama hicho hutoa mafunzo endelevu kwa wanachama wake ili kuongeza uelewa na ufanisi wa kiutendaji, badala ya kutegemea waajiri pekee.
Junus alieleza kuwa TPBA ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 16A (1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268, pamoja na Tangazo la Serikali Na. 589 la tarehe 16 Agosti 2019.
Aidha, alifafanua kuwa TPBA ni tofauti na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambapo TPBA uwakilisha wanasheria wa Serikali, wakati TLS hujumuisha wanasheria wote nchini, bila kujali mwajiri.
Alisema kuwa chama wa TPBA unategemea ajira ya mwanachama katika utumishi wa umma, wakati TLS huruhusu wanachama wake kuendelea hata baada ya kutoka kazini.
Akizungumza kwa niaba ya wahariri walioshiriki kikao kazi hicho, Mhariri Mkuu wa Clouds Media, Joyce Shebe, alipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuratibu kikao hicho ambacho kimetoa maarifa na uelewa kuhusu masuala ya kisheria kwa wahariri, jambo litakalosaidia kuboresha utekelezaji wa majukumu yao.
“Tunathamini nafasi hii ya kushirikishwa katika kujadili masuala ya sheria ambayo ni msingi wa kazi zetu. Tunatarajia ushirikiano huu uendelee,” alisema Shebe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.