RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa Kuzindua Kitabu cha Mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 jijini Dodoma kesho (tarehe 14 Septemba, 2021).
Hayo yamesemwa leo, Septemba 12, 2021 jijini Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa tukio hilo ambapo amesema linalenga kuandaa umma na wadau kwa ujumla kwa ujio wa sensa ya watu na makazi ya mwaka ujao.
Amesema uzinduzi huo unaokwenda na kauli mbiu inayosema "Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa", utafanyika kesho Septemba 14 katika Uwanja wa Jamhuri jijini hapa kuanzia saa 1 asubuh na utahudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa kamati ya Kuu ya sensa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) na Mwenyekiti mwenza kutoka Zanzibar, Makamu wa pili wa Rais, Mhe. Hemed Suleiman Abdallah.
Amewataja viongozi wengine kuwa ni Kamisaa wa Sensa Tanzania Bara, Anna Makinda, Kamisaa wa Sensa Zanzibar, Balozi Mohamed Haji Hamza, pamoja na Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu wakuu, Manaibu katibu wakuu na viongozi wa Serikali kutoka Mikoa minne.
“Viongozi wa serikali kutoka Mikoa minne watashiriki, Mkoa wa Singida, Iringa, Morogoro na Manyara hivyo hata wananchi wa Dodoma wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kumuunga mkono Rais wetu kwasababu sensa ni jambo letu wote, ” alisema Mtaka.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Takwimu, Daniel Masolwa amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo ina jukumu la kuratibu masuala ya sensa hivyo tayari imeshaandaa sensa ya majaribio ambayo tayari inafanyika Katika Mikoa 13.
Alisema kuwa lengo la sensa ya majaribio ni kupima na kuhakiki vitendea kazi ili kama vitakuwa na changamoto virekebishwe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.