CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kimetakiwa kuhakikisha kinaendelea kutetea maslahi ya wafanyakazi pamoja na kuwaandaa watumishi wa umma kabla ya kustaafu kujua wanatakiwa kufanya nini mara baada ya kustaafu.
Akizungumza leo jijini Dodoma Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka katika mkutano Mkuu wa TALGWU, amesema yeye wito wake kwa chama hicho ni kuendelea kutetea maslahi ya wafanyakazi nchini kwenye mambo ya msingi.
“Wito wangu kwenu tusimamie maadili ya watumishi tuwatetee kwenye mambo ya msingi hata kwenye gharama za kesi fanyeni zile zenye mantiki ilimuache alama,” amesema.
Pia, amekitaka chama hicho, kuwaandaa watumishi kabla ya kustaafu ili wajue wanatakiwa kufanya nini mara baada ya kustaafu kwani baadhi wamekuwa wakitapeliwa mara baada ya kustaafu.
Vilevile amewataka kuwa na malengo yanayoishi ikiwemo kuweka vitega uchumi ambavyo vitawasaidia katika kujiendesha. “Lazima muwe na malengo mnayoyaishi sio muda wote mpo Mahakamani hii inaharibu tengenezeni vitu vizuri ambavyo vitawaonesha,” amesema Mtaka.
Pia, amewataka kuwapa maelezo ya kutosha watumishi wapya ili wajue umuhimu wa chama hicho kwani wengi wamekuwa wakidanganywa kuhusiana na chama hicho.
“Hawa wanaoajiriwa wanasema chama cha nini hakuna ambaye ameelimishwa kuhusiana na bima na mafao lakini lazima kuwe na utaratibu wakufanya semina hii itasaidia sana,” amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa wa Dodoma.
Adiha, Mtaka amewataka kuwekeza Mkoani humo katika sekta ya ardhi kwani kuna fursa nyingi. “Hapa ni Makao Makuu ni kama unavyoenda Dar unakuta mtu ana ekari mbili Mikocheni unajiuliza alipataje. Nawaomba pata muda, Dodoma chumba na sebule 200,000 si kitu kibaya huu muda ambao mpo hapa mpate ka-ardhi kadogo,” alifafanua zaidi.
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Mara, Magreth Shau amesema wataendelea kufanya kazi kwa weledi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wafanyakazi ili wasikope mikopo inayoumiza.
“Kwa niaba ya wafanyakazi tunashukuru yapo mengi umetuasa, kikubwa umetuasa tuwe watumishi tunaosikiliza na kusimamia, tunaenda kufanya uchaguzi ambao utakifanya chama chetu kiwe imara zaidi. Tunakuahidi sisi kwa kuanzia katika ngazi za Mikoa tutaenda kulisimamia suala la utoaji wa elimu kwa watumishi wenzetu wasiharibiwe na mikopo umiza,” amesema Mwenyekiti Shau.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.