Na Noelina Kimolo, DODOMA
SERIKALI mkoani Dodoma imewahakikishia wazee kuwa itaendelea kusimamia sera ya wazee kwa lengo la kuwahakikishia upatikanaji wa huduma bora kwa ustawi wa maisha yao kutokana na mchango wao mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Hakikisho hilo lilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Khamis Mkanachi alipomwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka, katika hafla fupi ya uzinduzi wa Baraza la Wazee la Mkoa huo lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Mkanachi alisema kuwa serikali kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003 imeeleza kuwa wazee ni kundi muhimu katika jamii na wanapaswa kutambuliwa na kupewa fursa ya kushiriki katika mambo yanayohusu maisha ya kila siku kwa manufaa ya watanzania wote. Vilevile, inahakikisha wazee wanapata huduma zote muhimu ambazo zitawawezesha kushiriki kwa ukamilifu katika maisha ya kila siku.
“Serikali inaendelea kuwahudumia wazee katika upande wa afya, lishe na huduma zote za msingi ili kukidhi mahitaji ya mwanadamu huu ni wajibu wa msingi ambao serikali yetu imeuchukua” alisema Mkanachi.
Akiongelea uongozi wa baraza la wazee uliochaguliwa, alisema kuwa unawajibu wa kuwasaidia na kuwatetea wazee ili waweze kusimamia haki na ustawi katika kupewa kipaumbele kwenye huduma mbalimbali.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Nathalis Linuma alisema kuwa anatambua msaada utolewao na wazee kwa kuwa hata viongozi wengi kabla ya kufanya maamuzi huwa wanawashirikisha wazee katika maamuzi yao.
“Na utamaduni huo umekuwa ukiendelea kila siku na ndio maana hata sisi tukaona ni muhimu kuwa na Baraza la Wazee katika kuleta maendeleo ya taifa’’ alisema Linuma.
Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo alisema kuwa ni muhimu kwa wazee kujua haki zao katika kufanya maamuzi ili kuleta maendeleo katika jamii.
“Sisi wazee tunayo mambo mengi ambayo serikali tunahitaji mtusaidie. Wazee waliochaguliwa kuanzia ngazi ya Kata hadi Mkoa hawajui kazi yao na mipaka hivyo, tumeomba kupewa semina za mabaraza ya wazee ili watambue wajibu wao katika kazi zao” alisema Mchungaji Mpolo.
Pia ameomba Halmashauli ziwe zinatenga bajeti za kuwawezesha wazee kutekeleza majukumu yao kuanzia ngazi za chini hadi juu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.