Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka ameahidi kukutana na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kujadilia namna ya kuwawezesha Wafugaji wa Mkoa wa Dodoma kunufaika na shamba la Serikali lililopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma maarufu kama 'Kongwa Ranch'.
Mhe. Mtaka amesema atazungumza na Wizara ya Mifumo na Uvuvi ili wawapatie Wakulima wa Dodoma, vitalu vya ardhi kwenye shamba hilo la Mifugo la Serikali lenye ukubwa wa Hekta 38,000 (sawa la Ekari 95,000) kwa utaratibu wa kukodisha ili wakulima hao waweze kupata maeneo ya kuendeshea shughuli za ufugaji wa kisasa na uoteshaji malisho ya mifugo.
Aidha, Mhe. Mtaka amesema kuwa kiaumbele chake katika sekta ya ufugaji kwenye Mkoa wa Dodoma ni kuendesha ufugaji bora, wa kisasa, wenye tija na mazao ya mifugo kama vile Nyama, Maziwa, Ngozi, Pembe na kwato.
Mtaka ameyasema hayo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akifungua mkutano wa Wafugaji wa Mkoa wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma. Wafugaji hao katika risala yao waliyoisoma kwa Mkuu wa Mkoa Mtaka, wamemlalamikia kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maeneo ya kufugia na maeneo ya malisho na kwamba maeneo mengi yaliyopo yana changamoto ya migogoro ya mipaka, ukosefu wa mipango ya matumizi bora ya ardhi, ukosefu wa huduma muhimu kama maji na majosho ya kuogeshea mifugo.
Akisoma risala ya Wafugaji, Katibu wa Chama cha Wafugaji wa Dodoma, Reginaldo Lubeleje amesema kuwa baadhi ya maeneo ya ufugaji na malisho yamekuwa yakivamiwa kwa shughuli za kilimo. Aidha, wafugaji bado wana ukosefu wa elimu ya kutosha ya ufugaji bora na kuongeza kuwa kwa hapa Dodoma lipo shamba kubwa la mifugo la Serikali Wilayani Kongwa (Kongwa Ranch) lakini halina mchango katika kuwasaidia wafugaji wa Dodoma na kubadili aina ya ufugaji wao kuwa bora na wa kisasa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.