NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Chande, amesema kuwa Serikali imeweka udhibiti wa mianya ya rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma uliosababishwa na kasoro katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (TANEPS) kwa kufanya maboresho makubwa ya mfumo huo.
Hayo yamebainishwa mkoani Iringa wakati alipofanya ziara ya kukagua maboresho ya mfumo huo yanayofanywa na wataalamu wa ndani kwa lengo la kuondoa changamoto zilizopo na kukidhi mahitaji halisi ya Serikali na wazabuni.
Chande alisema kuwa kumekuwa na changamoto ya kupata thamani halisi ya fedha katika huduma na bidhaa kutokana na mianya ya rushwa iliyokuwepo katika mfumo wa manunuzi ambayo inasababisha utofauti mkubwa wa gharama kwenye eneo moja.
"Kumekuwa na usiri mkubwa katika michakato ya ununuzi, hali inayofanya mtu ajiulize huu usiri una nini katikati yake, ununuzi unatakiwa ufanyike kwa uwazi na haki hivyo wataalamu mnaofanya maboresho haya mnaweza kututengenezea mfumo unao akisi uhalisia katika ununuzi na utakaosaidia manunuzi kufanyika kwa haki" alisema Chande.
Alisema kuwa nia ya Serikali ya kufanya maboresho hayo ni kuhakikisha taasisi nunuzi zinatoka katika mazoea ya kufanya michakato ya ununuzi nje ya mfumo kwa kuwa ununuzi wa nje ya mfumo unaongeza uwezekano wa rushwa na upotevu wa thamani ya fedha.
Aidha, Chande alisema zipo faida nyingi ambazo Serikali itazipata baada ya maboresho hayo kukamilika ikiwemo kuimarika kwa uchumi wa nchi kwa kuokoa mapato ya Serikali yanayopotea kwa kuwa asilimia 70 ya matumizi yote ya bajeti ya nchi yameelekezwa katika ununuzi.
Pia alimtaka Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakumu Maswi, kuhakikisha wote wanaotakiwa kutumia mfumo huo wanautumia, kwa kuwa itasikitisha kuona wataalamu wanatumia muda na nguvu zao katika kufanya maboresho ya
mfumo halafu wengine wanakaidi kuutumia.
Chande ameipongeza PPRA kwa juhudi wanazoendelea nazo za kusimamia maboresho makubwa katika mfumo wa ununuzi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika Sekta ya Ununuzi nchini
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.