Na. Dennis Gondwe, DODOMA
SERIKALI ya awamu ya sita kutoa msamaha wa kodi kwenye nyasi bandia hadi ngazi ya halmashauri na kuweka nyasi hizo katika kiwanja cha michezo Dodoma.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa kuwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/2023 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba.
“Nichukue nafasi hii kuwahakikishia watanzania kuwa tutaweka nyasi bandia kwenye viwanja vitano kwa kuanzia Mwanza, Arusha, Tanga, Dodoma na Mbeya ili kukuza michezo hapa nchini. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 msamaha wa kodi kwenye nyasi bandia na vifaa ambata vyake utakwenda mpaka ngazi ya halmashauri” alisema Dkt. Nchemba.
Waziri wa Fedha alisema kuwa serikali itarudisha michezo ya bahati nasibu ya taifa kupitia sekta binafsi. “Sambamba na hiyo serikali kupitia Bodi ya michezo ya kubahatisha, TRA na sekta binafsi wataanza kuendesha bahati nasibu kwa kupitia risiti za EFD ili kuchochea wananchi kudai risiti wanaponunua bidhaa. Serikali itatumia sehemu ya michango ya wajibu wa kampuni kwa jamii kwa kiwango kisichozidi asilimia mbili kwa ridhaa ya waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha ili kuendeleza michezo nchini.
Aidha, waziri aliipongeza timu za Serengeti girls na Tembo warriors kwa kukata tiketi za kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya dunia. “Niitakie kila la heri timu yetu ya Taifa stars ambayo bado iko kwenye kampeni za kutafuta tiketi ya mashindano ya kimataifa” alisema Dkt. Nchemba.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.