SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali watoa huduma wa sekta ya Afya na kuthamini huduma wanazotoa kwa wananchi katika kuelekea kipindi cha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alipokuwa akiongea na wafanyakazi wa Kituo cha Afya Makole katika kuelekea kilele cha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Alhaj Shekimweri alisema “tunaposherehekea Uhuru wa nchi yetu, hawa wanaohudumiwa ni watanzania wenzetu ambao wapo huru. Hivyo, tunawajibu wa kuwasaidia ili wajifungue wakiwa salama na wengine wanaopata huduma mbalimbali za Afya. Serikali ya awamu ya sita inawajali na milango yetu ipo wazi kuwasikiliza pale mtakapohitaji kusikilizwa. Najua Mganga Mkuu, Dkt. Andrew Method anafanya kazi vizuri na sisi tunamtegemea sana na anawaunganisha vizuri. Najua mpo salama kwenye mikono yake na Mganga Mfawidhi, Dkt. Revocatus Baltazar. Nachukua nafasi hii kutambua, kuthamini na kuwapongeza kwa kazi nzuri, hongereni sana”.
Aidha, alimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwenye sekta ya Afya kuanzia mishahara, miradi, vifaa tiba, kinga na vitendanishi. “Ukiwa taifa huru moja ya mambo yanaoonesha ni uwezo wa kutibu wananchi wako. Nimefika hapa kuwaona wagonjwa kina mama waliojifungua na tumepata mrejesho wa huduma nzuri na wanazifurahia. Ukiona wanafurahia hizi huduma hazifanywi na roboti zinafanywa na wanadamu ambao ndiyo ninyi. Niwaombe muendelee na huduma hizo mnazotoa kwa weledi na upendo” alisema Alhaj Shekimweri.
Katika kuelekea miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Wilaya ya Dodoma ilitembelea Kituo cha Afya Makole kukagua hali ya utoaji huduma katika wodi ya kima mama, kuwatia moyo kina mama wanaotarajia kujifungua na waliojifungua na kuwapatia zawadi mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.