WATOTO 40 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na mishipa ya damu wamefanyiwa upasuaji kwenye kambi maalum ya matibabu iliyomalizika jana katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Mending Kids la nchini Marekani.
Kwa watoto hawa kufanyiwa upasuaji huu hapa nchini Serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni moja fedha ambazo zingelipwa kama upasuaji huo ungefanyika nje ya nchi.
Akizunguma za waandishi wa habari jana jijini Dar Es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema kati ya watoto 40 waliofanyiwa upasuaji 20 walifanyiwa upasuaji wa kufungua Kifua na 20 walifanyiwa upasuaji kwa njia ya tundu dogo kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Dkt. Kisenge alisema tangu waanze kushirikiana na shirika hilo la Mending Kids jumla ya kambi sita za matibabu ya moyo kwa watoto zimeshafanywa huku wataalamu wa JKCI wakifundishwa njia mbalimbali za kufanya upasuaji wa kufungua kifua na ule wa tundu dogo kwa utaalam zaidi.
"Kupitia Shirika la Mending Kids wataalam wa JKCI wa upasuaji wa moyo kwa watoto wamekuwa mabingwa wabobezi katika kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto wenye magonjwa ya moyo hivyo kutufanya kuwa mabingwa kusini mwa jangwa la Sahara katika kutoa huduma bora za matibabu ya moyo kwa watoto," alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge pia alisema shirika la Mending Kids limetoa msaada wa vifaa vya matibabu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete vyenye gharama ya dola za kimarekani milioni 1.2 ikiwa ni sehemu ya kusaidia watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa Moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema kwa mara ya kwanza tangu waanze kufanya upasuaji wa moyo hapa nchini wameweza kufanya upasuaji maalum (high bridge procedure) unaohusisha upasuaji wa aina mbili (kwa wakati mmoja) ule wa kufungua kifua na upasuaji wa tundu dogo kwa kufungua kwa tundu dogo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.