SERIKALI ilitoa Shilingi Bilioni 263 ya fedha za ahueni ya UVIKO-19 ili kuboresha Hospitali za rufaa za mikoa kati ya fedha hizo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma ilipewa kiasi cha bilioni 4.6 ambazo zimeweza kujenga jengo la wagonjwa mahututi (ICU) litakalokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 50 kwa wakati mmoja pamoja na ununuzi wa vifaa tiba.
Hayo yamebainiashwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipotembelea Hospitali hiyo kujionea utekelezaji wa fedha hizo ambapo kunajengwa jengo la wagonjwa mahututi (ICU), jengo la Radiolojia (CT-Scan), nyumba ya mtumishi pamoja na ukarabati wa jengo la huduma za dharura (EMD).
Amesema kwa kuwa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) linaendelea vizuri, litasaidia kuongezeka kwa vitanda vya wagonjwa mahututi hadi kufikia wagonjwa 50 kutoka wagonjwa 18 wa sasa.
“Fedha hizi tulizowezeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan, sasa Wizara ya afya kipaumbele chetu ni ubora wa huduma, hivyo kutokana na vitanda hivyo tutaweza kuwahudumia wagonjwa mahututi 50 ikiwa ni utekelezaji wa maono na dhamira ya Mheshimiwa Rais”. Amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema kwa jengo la Radiolojia ambalo litawekwa mashine ya CT-Scan ambapo huduma hiyo haikuwepo hapo awali, itawezesha kupunguza mzigo kwa wakazi wa Dodoma ambao walikuwa wanaenda kupata vipimo hivyo kwenye hospitali ya Benjamini Mkapa.
“Hospitali hii kwa mwezi wanapata wagonjwa 75 hadi 100 ambao wanapaswa kufanyiwa kipimo cha CT-Scan, hivyo huduma hii itawawezesha wananchi kupata kwa bei rahisi na kuwaondolea usumbufu hadi hospitali ya kanda ya Benjamini Mkapa.” Aliongeza Waziri Ummy.
Kwa upande wa ukarabati wa jengo la huduma la dharura (EMD) Waziri Ummy amesema huduma zote za dharura zitapatikana katika eneo moja hivyo Serikali imeweza kuboresha huduma za wagonjwa wa dharura kwani kutokuwa na huduma hizo unaweza kupoteza maisha ya watu.
Waziri Ummy Mwalimu akiongea na baadhi ya wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma 'General' ili kupata huduma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.