Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo amesema serikali imeamua kukarabati shule ya Sekondari ya Bihawana ili kuweka katika mazingira bora ya mwanafunzi kujifunzia.
Waziri Jafo ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika shule ya Bihawana iliyopo katika Manispaa ya Dodoma na kukagua miundombinu ya shule hiyo kabla ya ukarabati mkubwa unaotarajia kuanza hivi karibuni. Katika ziara hiyo Waziri Jafo alifuatana na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma Prof. Davis Mwamfupe, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bi. Hidaya Maeda na maafisa wengine.
Akielezea lengo la ziara yake Waziri Jafo amesema ni kukagua uchakavu wa majengo wanayotumia wanafunzi na kupata maelezo kutoka kwa Mhandisi Mshauri kile wanachotarajia kufanya baada ya kufanya tathmini ya kina juu ya kinachohitajika katika kazi ya ukarabati wa shule hiyo.
Waziri Jafo amesema baada ya kufanya ukaguzi wa maeneo mbalimbali ya shule amegundua kuwa kunauchakavu mkubwa wa mabweni, ofisi ya waalimu, madarasa, bwalo, jiko na pia uchakavu mkubwa kwenye vyoo pamoja na ukosefu wa maji katika shule hiyo.
Waziri Jafo amesema serikali imepanga kuibadilisha shule ya Sekondari ya Bihawana na kuwa ya kisasa ili kuwa kivutio kwa wazazi kuwaleta watoto wao katika shule za Sekondari,na kuwafanya wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga hapo kuona fahari kupata Elimu yao katika mazingira bora na rafiki kwa kujifunzia.
“Ninataka kuibadilisha shule ya Sekondari ya Bihawana kuwa shule yenye Kuvutia kiasi ambacho Walimu watafanya kazi katika mazingira bora, watumishi wa hapa na wanafunzi pia na zaidi wale wanafunzi waliosoma hapa miaka ya nyuma wakija shuleni hapa wapotee kwa kukuta mazingira tofauti na yale waliyo yaacha” amesema Jafo.
Shule hii iko katika mpango wa Serikali wa Uboreshaji miundombinu ya Shule kongwe 89 na Shule hii inaanza kukarabatiwa katika awamu ya pili ya mpango huu na Ukarabati huo utagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.2.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.