Na. James K. Mwanamyoto
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amewataka wasimamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa shule za Sekondari maalum 26 za wasichana za mikoa, kuhakikisha wanasimamia vizuri matumizi ya fedha zilizotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kujenga shule hizo ili ziwe na viwango bora vitakavyowawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.
Mhe. Katimba ametoa maelekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa, alipoitembelea Shule Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha ujenzi wa shule hiyo ambayo imejengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
“Nimeridhishwa na kiwango cha ujenzi wa shule hii Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma ambayo ilipokea fedha za Mhe. Rais Samia kiasi cha shilingi bilioni 3 katika awamu ya kwanza awamu ya kwanza shilingi bilioni 3 na awamu ya pili itapelekwa bilioni 1.1,” Mhe. Katimba ameeleza.
Aidha, Mhe. Katimba ametoa wito kwa Wakurugenzi wengine wa Halmashauri nchini wanaosimamia Ujenzi wa Shule za Sekondari Maalum za Wasichana katika mikoa mingine, kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu hiyo ya shule iliyojengwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuunga mkono jitihada zake.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais, na ni wazi kuwa anafanya jitihada za makusudi ambazo zinazoonekana na ushaidi ni hii shule Maalum ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma yenye maabara, mabwalo, mabweni, madarasa na nyumba za walimu zenye viwango bora kabisa,” Mhe. Katimba amesisitiza.
Kwa upande wake Bw. Khamis Rajabu ambaye ni Mkazi wa Uvinza mkoani Kigoma amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa shule hiyo ya wasichana mkoani kigoma, ambayo imetatua changamoto iliyokuwa ikiwakabili ya watoto wa kike kukosa shule ya sekondari yenye viwango bora.
Naye, Odetha Denis ambaye ni Mwanafunzi wa Shule Maalum ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Kigoma, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua thamani ya watoto wa kike na kuwajengea shule maalum kwa ajili yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.