KATIKA kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na uzalendo na kuwatambua mashujaa wote serikali imesema somo la Historia ya Tanzania litaanza kutumika kwa lazima kuanzia mwezi Julai Mwaka huu
Kauli hiyo imetolewa juzi Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Wizara ya Elimu Dodoma.
Profesa Ndalichako amesema katika kuzingatia maelekezo ya Rais wa Tanzania Dkt.John Magufuli, Somo hilo la Historia lisomwe na wanafunzi wote na mihtasari imeandaliwa kusoma somo hilo la Historia kuanzia Elimu ya awali na kuendelea kwa ulazima.
Aidha amesema Wizara inaendela kushirikiana na wadau mbalimbali kuchapisha vitabu na vitakamilika mwezi Machi mwaka huu ambapo somo hilo litaanza kufundishwa Mwezi Julai, 2021.
Katika hatua nyingine Profesa Ndalichako amebainisha kwamba Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inashirikiana na wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo katika uandaji wa mihtasari.
"Nasisitiza watunzi wa vitabu lazima wahakikishe wanaandika kwa ufasaha hivyo sisi kama Wizara tunashirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika kuandika," amesema Profesa Ndalichako.
Ikumbukwe kuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati akiapisha Mawaziri na Naibu Mawaziri Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma mnamo tarehe 9 Desemba 2020 aliagiza Somo la Historia ya Tanzania lianze kufundishwa mashuleni ili kujenga uzalendo na kuwafanya wanafunzi kujua walikotoka.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.