WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt.Faustine Ndugulile,amezindua studio za TBC Redio Jamii Kanda ya Kati ambazo zimefadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC).
Akizungumza leo Julai 26,2021 jijini Dodoma mara baada ya uzinduzi huo Waziri Ndugulile,amesema kuwa lengo la kuzindua studio hizo ni kuboresha usikivu wa Radio Kanda ya Kati.
”Niwapongeze UCSAF na TBC kwa ushirikiano wenu huu wa kuanzisha Redio Jamii ambayo sasa itakuwa na manufaa kwa wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Kati, niwahakikishie kama Wizara tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuleta usikivu wa mawasiliano,” Amesema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt.Ndugulile amesema kuwa Serikali imetangaza zabuni ya leseni na masafa na kuwa tayari imetenga shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuboresha usikivu.
“Tayari tumeshatangaza zabuni ya leseni na masafa katika maeneo ambayo hayana usikivu wa redio, tunawaombea Wananchi wenye nia ya kuwekeza watumie fursa hiyo,” amesema.
Aidha, Dkt. Ndugulile amesema serikali pia itafanya mapitio ya tozo za Redio kwenye Wilaya na maeneo ya mipakani ambapo itapunguza tozo hizo kwa lengo la kuongeza usikivu kwenye wilaya hizo.
Pia Dkt. Ndugulile ametoa wito kwa watanzania kufika kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano TCRA ili kuangalia Wilaya ambazo tenda hizo zimetangazwa ambapo zitaenda sambamba na punguzo la leseni kwenye Redio hizo.
Kwa upande wake Naibu waziri, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul, amesema kuanzishwa kwa redio hiyo ni jambo la kihistoria kutokana na uhumimu wake kwa Taifa hasa katika kufikisha huduma za matangazo ya redio kwa wananchi wa Makao Makuu na mikoa ya jirani.
“Kituo hiki kimefunguliwa leo tunategemea masuala ya kawaida yanayowagusa watanzania yanakwenda kuzungumzwa na burudani mbalimbali zinaenda kutolewa pamoja na vipindi vinavyokwenda kurushwa ni vya utalii, kilimo na ufugaji, michezo, vijana, muziki, mila na desturi,” amesema Waziri Gekul.
Aidha, ametoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuzingatia weledi na kuhakikisha maudhui yanayokwenda kwa wananchi hayapotoshi na ni sahihi na kweli.
Awali Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba amesema gharama halisi ya ukarabati na ununuzi wa vifaa vya Radio Jamii hiyo ni Shilingi Bilioni 1.71 huku TBC wenyewe wakichangia Shilingi Milioni 163.
Mashiba amesema uzinduzi wa Radio hiyo ni muendelezo wa Mfuko huo kurahisisha mawasiliano ambapo awali walishafanya hivyo jijini Arusha na leo ni zamu ya Dodoma.
”Tarehe 30 tutazindua kituo kingine cha kurusha matangazo katika eneo la Kisaki ambacho pia tumekifadhili sisi lengo ni kuhakikisha Radio yetu ya Taifa inasikika kila kona.
“Sisi na TBC tumeendelea kushirikiana kutekeleza miradi ya upanuzi wa usikuvu wa Mawasiliano wenye lengo la kupeleka huduma ya habari kwa wananchi kwa njia ya redio” amesema Mashiba.
Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Rioba amesema kuwepo kwa Redio hiyo, kutasaidia katika kurusha habari za kikanda ili kukuza uelewa wa wananchi kuhusiana na masuala ya kijamii katika maeneo yao.
”Redio hii itaongeza uwezo wa kuandaa vipindi vinavyohusu matukio ya kitaifa ikiwemo vikao vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kurusha vipindi vya runinga kutokea Dodoma ikiwemo vipindi vya Jambo Tanzania na TBC Aridhio” amesema Dkt.Rioba
Hata hivyo Dkt. Rioba ameishukuru UCSAF kwa ufadhili huo na kuwataka wananchi wa Dodoma na Mikoa jirani kuitumia Redio hiyo kama fursa ya kujikwamua kiuchumi, kielimu na kijamii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.