MKURUGENZI wa TEHAMA wa Wizara ya Afya Haji Bamsi ameshauri kutumia tovuti za hospitali zilizoanzishwa kutangaza kazi kubwa ya kuokoa maisha inayofanywa na hospitali.
Bamsi ameyasema hayo katika mafunzo ya siku tano ya utengenezaji wa tovuti za hospitali kwa maafisa TEHAMA wa hospitali za rufaa za mikoa na hospitali tano za Halmashauri za Wilaya yanayofanyika mjini Morogoro.
Amesema kuna mambo mengi ambayo yanafanyika katika vituo vya kutolea huduma za afya lakini hayapati nafasi ya kutangazwa katika vyombo vya habari.
"Vyombo vingi vya habari vimekuwa vinatangaza habari mbaya zaidi zinazotokea katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuacha habari nzuri zinazoweza kuleta matokeo makubwa kwa wananchi" alikazia Bamsi.
Bamsi amesema kuwa "Tovuti hizi za hospitali zisaidie kutangaza mambo mazuri mengi yanayofanywa na hospitali ili yaweze kufahamika kwa wananchi ikiwemo kutoa elimu kwa umma katika masuala mbalimbali ya afya".
Kuna habari nyingi ambazo zinaendelea katika hospitali ikiwemo miradi mbalimbali ya afya, elimu ya magonjwa mbalimbali, kuelimisha kuhusu Bima ya Afya na CHF iliyoboreshwa, ambazo hazipati nafasi ya kutosha kutangazwa katika vyombo vya habari.
Akisisitiza zaidi amesema kuwa tovuti zilizoanzishwa zikitumika vizuri zitasaidia wananchi wengi kupata taarifa nyingi za afya ambazo pia zinaweza kusambazwa katika mitandao ya habari kutoka katika tovuti na kuwafikia wananchi wengi.
“Hatutaki kusubiri kutangaza habari za hospitali kwa matukio mfano kuzaliwa watoto, hadi iwe siku ya sikukuu ndiyo zinatangazwa, wakati hopsitali zinafanyakazi kubwa ya kuzalisha watoto na kuokoa maisha ya watu kila siku" anasisitiza Mkurugenzi Bamsi.
Mafunzo ya utengenezaji tovuti za hospitali yameratibiwa na OR-TAMISEMI na kuwashirikisha maafisa TEHAMA 65 kutoka katika hospitali za Rufaa za mikoa 28 na maafisa TEHAMA watano kutoka katika hospitali tano za Halmashauri nchini.
Chanzo: tovuti ya Halmashauri ya Songea
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.