Na. Anna Stanley, DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamedi Mchengerwa ametoa tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka na uchaguzi utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Mchengerwa aliyasema hayo katika viwanja vya Chinangali park, jijini Dodoma wakati akizungumza na wananchi na kuwahamasisha kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa na kujitokeza kupiga kura.
"Tangazo hili limetolewa chini ya Kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka, 2024 pamoja na matangazo ya serikali Na. 571, Na. 572, Na. 573, Na. 574 ya mwaka 2024" alisema Mchengerwa.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 145 na Ibara ya 146, inaeleza uwepo wa Serikali za Mitaa pamoja na madhumuni yake ambapo miongoni mwa madhumuni ni pamoja na kupeleka madaraka kwa wananchi, alisema.
“Sheria za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya, sura Na. 287 ya Serikali za Mitaa, Mamlaka kamili, sura Na. 288 zinaelekeza kufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lengo ni kufanya serikali za mitaa ziongoze kidemokrasia. Kwa mujibu wa kifungu cha 201 ‘A’ cha Sheria za Serikali za Mitaa Mamlaka za Wilaya, sura Na. 287 na kifungu Na. 77A, huongoza uchaguzi huo wa serikali za mitaa, na viongozi wanaochaguliwa katika ngazi hii ni, wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa halmashauri ya vijiji, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji, wagombea wote katika ngazi mbalimbali za uongozi wanatakiwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu" alisema Mchengerwa.
Uchaguzi wa mwisho wa serikali za mitaa ulifanyika mwezi Novemba, 2019. Hivyo, uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika mwezi Novemba, 2024, uandikishaji na uandaaji wa orodha ya wapiga kura utaanza siku 47 kabla ya tukio la uchaguzi, aliongeza.
Kwa tangazo hilo, wananchi wote wanaobwa kujitokeza kwa ajili ya kujiandikisha kupiga kura, kugombea na kushiriki katika uchaguzi huo ili kupata viongozi wa serikali za mitaa kwa maendeleo ya nchi wakati kampeni zitaanza tarehe 20–26 Novemba, 2024 na uchaguzi utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
MWISHO.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.