WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Januari 16, 2022 amekagua maendeleo ya ujenzi wa Ikulu inayojengwa katika eneo la Chamwino, Jijini Dodoma na kusema ameridhishwa na kasi ya ujenzi na ubora wa majengo hayo na amemtaka mkandarasi ahakikishe mradi huo unakamilika mwezi Mei mwaka huu.
Waziri Mkuu amewasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati na kuwapongeza wote wanaohusika na ujenzi. “Tunataka kumuwezesha Mheshimiwa Rais kufanya kazi katika eneo lake maalum na afanye kazi katika mazingira mazuri na kwa ufanisi.”
“Nimefurahishwa na taarifa kwamba ujenzi huu umefikia asilimia 91 na hatua iliyobaki hizi asilimia 9 ni kazi ndogondogo kama uwekaji wa milango, njia za mifumo ya hewa na umeme na zote zinaenda vizuri.” Amesema Waziri Mkuu na kusisitiza kuwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan pia anatarajia kuona ujenzi huo unakamilika kwa wakati.
Aidha, Waziri Mkuu amelipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kutekeleza ujenzi huo kwa ufanisi. “Ramani iliyoko hapa iko sawasawa na jengo la Ikulu lililoko Dar es Salaam, Wakandarasi wetu mmefanya kazi kubwa sana. Hii imedhihirisha kuwa nchi yetu ina wataalam wa kutosha kujenga aina yoyote ya majengo.”
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania, Mhandisi Daudi Kondoro amemhakikishia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba mradi huo utakamilika na kukabidhiwa mwezi Mei kama inavyotarajiwa kwani sasa uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.