Na. Dennis Gondwe, DODOMA
MRADI wa ujenzi wa nyumba ya walimu (mbili kwa moja) katika shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma utawasaidia walimu kukaa mazingira ya shule jambo litakaloongeza ufanisi katika utendaji kazi wao na kutoa matokeo chanya.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma, Mwl. Livinus Tanganyika alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu (two in one) katika Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma iliyopo Kata ya Hombolo Makulu Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mwl. Tanganyika alisema kuwa serikali kupitia mradi wa kuboresha shule za sekondari (SEQUIP) ilitoa jumla ya shilingi 95,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya walimu ambapo lilikuwa ni hitaji kubwa kwa sababu eneo la shule liko mbali na eneo la makazi ya watu. Fedha za ujenzi ziliingizwa katika akaunti ya shule tarehe 20/6/2023 na kuvuka mwaka na kuanza kutumika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Akiongelea utekelezaji wa mradi huo alisema kuwa ulianza tarehe 9 Septemba, 2023 baada ya taratibu za manunuzi kukamilika na ujenzi unatekelezwa kupitia ‘force account’. “Mradi huu unahusisha ujenzi wa nyumba moja ya walimu (two in one) yenye vyumba vitatu, sebule, jiko na stoo kwa kila nyumba. Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 99 ikiwa bado milango michache ambayo ipo kwa fundi katika hatua ya umaliziaji pamoja na ufungaji wa vyoo viwili vya kukaa. Mradi unategemea kukamilika kabla au ifikapo tarehe 25 Novemba, 2023 tayari kwa matumizi” alisema Mwl. Tanganyika.
Kuhusu faida za mradi ukikamilika, alizitaja kuwa ni walimu kukaa kwenye mazingira ya shule na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji kazi. Nyingine ni kuwezesha mazingira mazuri ya kuishi kwa walimu, aliongeza.
“Uongozi wa Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma unapenda kutoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha hizi ambazo zinaenda kuboresha maisha ya walimu. Pia tunatoa shukrani kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa maelekezo na usimamizi wa karibu wa miradi yote inayotekelezwa katika Jiji la Dodoma. Hii yote ni katika kuhakikisha kwamba Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inatekelezwa kwa vitendo” alisema Mwl. Tanganyika.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa Shule ya Shule ya Sekondari Mtemi Chiloloma umetumia kiasi cha shilingi milioni tisini na nne laki nane na elfu ishirini na tatu (94,823,000.00) hadi wakati kamati ya Siasa ya Mkoa wa Dodoma kuitembelea.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.