KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi (pichani juu), ametoa rai kwa wadau wote kushirikiana kwa pamoja kutafuta suluhu za changamoto za kiuchumi zinazovigusa vyombo vya Habari.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Dar es Salaam leo alipokuwa akifungua semina ya wadau iliyoandalilwa kati ya Wizara na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu na Sayansi (UNESCO) kutengeneza vipaumbele vya sekta hizo vitakavyoingia katika Mipango ya kitaifa na kimataifa hasa katika utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Dunia (SDGs).
“Mara chache sana tunapofanya semina na makongamano tunakumbuka kutathmini hili kwamba uhuru wa kiuchumi wa wanahabari ni muhimu sana. Mwanahabari ambaye analipwa kiduchu, hana uhakika wa mshahara, hana bima, hana pensheni kabla hajaenda kutafuta stori tayari hana uhuru. Semina hii ilete mapendekezo namna gani vyombo vya Habari viimarishe mapato yao na uchumi wao uimarishwe na pia ni muhimu mkaangalia dhana ya baadhi vya vyombo vya Habari kuanzishwa kwa malengo ya mtu kisha akitimiza malengo hayo miaka miwili mitatu wanatasnia walioajiriwa wanaanza kutelekezwa na kubaki hoi. Leteni mawazo makini ili kile sisi Serikali tunachopaswa kuanzia kwa wadau wa sekta wenyewe kianzishwe,” ameahidi Dkt. Abbasi.
Katika semina hiyo ambayo ni maandalizi ya Siku ya Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yatakayofanyika Arusha Mei 3 mwaka huu, Dkt. Abbasi pia ametoa tuzo kwa wanahabari na wadau wa Habari wanawake waliotoa mchango muhimu ambao ni Eda Sanga, Penzi Nyamangumi na Joyce Kiria.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.