WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amewataka wafanyabiashara wa Mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa zinazojitokeza kwa kujenga miundombinu wezeshi kwa wawekezaji na wageni kwani baada ya Serikali kuhamia Jijini Dodoma kumekuwa na ongezeko la wageni kutoka sehemu mbalimbali Duniani.
Kijaji aliyasema hayo wakati wa Kikao kazi na wafanyabiashara wa Jiji la Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Jengo la Mkapa ambapo kikao hicho kimewahusisha wajasiriamali na wafanyabiashara pamoja na majukwaa yanayojihusisha na ujasiriamali.
Kijaji alisema uchumi imara wa Taifa upo mikononi wa sekta binafsi hivyo amewahimiza wafanyabiashara hao kutumia fursa zote zinazojitokeza iwe ni sekta binafsi au kutoka serikalini ili kuendelea kukuza uchumi wa nchi.
Aliwahimiza wajasiriamali kuwa waaminifu na Fedha zinazotolewa na Serikali kama sehemu ya mtaji ili kuwawezesha na wengine kupata hiyo fursa.
"Lazima tukubaliane na utaratibu uliowekwa uadilifu wetu, uaminifu wetu ni muhimu hakuna fedha za bure sehemu yeyote lazima uwe na uhakika wa fedha kurudi na mtu unae mpatia fedha hivyo tunatakiwa kumthibitishia Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo mtetezi wetu namba moja "ameeleza Kijaji
Kwa Upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule akitoa salamu za Mkoa amempongeza Waziri huyo kwa kukutana na kuzungumza na wafanyabiashara hao pamoja na kutatua changamoto na kero zilizokuwa kikwazo katika utekelezaji wa biashara zao.
Senyamule alisema Mkoa wa Dodoma upo tayari kupokea wawekezaji na kuongeza idadi ya viwanda ili kuongeza na kukuza mapato va Serikali na uchumi wa nchi va Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.