Na. Halima Majidi, DODOMA
Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo Jiji la Dodoma, wameishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kukarabati miundombinu ya Soko hilo na kuomba kuharakishwa uboreshaji wa soko ili waweze kuendelea na majukumu yao, kwa sababu soko hilo ndio soko mama la chakula.
Akizungumza katika hafla ya Utiaji Saini Mikataba ya Ujenzi wa Miradi ya TACTIC uliofanyika katika Bustani ya Chinangali Park, Mfanyabiashara wa Soko Kuu la Majengo, Rhoda Boyi, alipongeza juhudi za Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kuwashirikisha katika hatua zote za mradi "Tunatarajia kuwa sauti zetu zitasikilizwa n
kuzingatiwa ili kuhakikisha kuwa maboresho haya yanakidhi mahitaji yetu na kuboresha mazingira ya biashara" alisema Boyi.
Kwa upande wake Mohammedi, alifafanua changamoto watakazokumbana nazo katika kipindi chote cha ukarabati wa jengo hilo, ni pamoja na; kupoteza wateja, kuharibika kwa bidhaa kutokana na kuhamishwa katika sehemu zao za biashara pamoja na upungufu wa chakula kwasababu Majengo ni Soko linalotumika kama ghala kubwa la chakula Dodoma" watu walikuwa wanaweka "stock" watu walikuwa wanaleta bidhaa kwa wingi hivyo watapunguza, mteja amezoea akitoka Chaduru, UDOM na Mipango anaenda moja kwa moja Majengo hivyo, kuhama sehemu moja kwenda nyingine kunatuathiri sana " alisema Mohammed.
Nae, Kaimu Katibu wa Soko Kuu la Majengo, Emanuel Samwel, alisema kuwa wapo tayari na wamepokea maboresho ya Soko hilo, na wameomba serikali kutoenda kinyume na makubaliano ya kwenye vikao mbalimbali vilivyokuwa vikiendelea.
Hata hivyo, Samwel alisema kuwa Soko la Majengo limejengwa mwaka 1993 nakuanza kutumika mwaka 1996 likiwa na wafanyabiashara 400, hivyo ni uhakika kuwa miundombinu ya Soko kwa sasa imechakaa, kupitia mkataba huu utaenda kuleta mabadiliko makubwa, "soko letu sisi ni soko mama, lina muda mrefi na kwa sasa lina watu 3200 -4000. Hivyo, ukiangalia idadi na muda soko lilipoanzishwa kiuhalisia tunashukuru serikali kwa kuona ukarabati huo" alisema Samwel.
Sambamba na hayo, uongozi huo uliahidi kutunza miundombinu ya Soko hilo pindi tu utakapokamilika kwa kuhakikisha wanawaelimisha wafanyabiashara wenzao kuhusu utunzaji wa miundombinu na kuimarisha usafi wa mazingira ya soko kwa ujumla kwa lengo la kuendelea kulipa thamani na hadhi Soko Kuu la Majengo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa (Mb), aliwahakikishia wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuwa serikali imejipanga kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati. "Tunaelewa changamoto mnazokabiliana nazo, na kupitia mradi huu, tunalenga kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wanaojihusisha na shughuli mbalimbali ili kuinua uchumi wa nchi kwa ujumla "alisema Mchengerwa.
Mchengerwa aliwataka viongozi wa ngazi zote wakiwemo Wakurugenzi, Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini( TARURA) na Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi hiyo kwa sababu imegharimu kiasi kikubwa cha fedha na pia imewalenga Watanzani "miradi hii inathamani kubwa, thamani ya miradi ni zaidi ya tirioni 1.1, ambapo mradi huu unaenda kuboresha miundombinu ya miji 45, niwaombe kwa pamoja muende mkasimamie miradi hii ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amewakusudia watanzania" alisema Mchengerwa.
Mradi wa uboreshaji wa Soko Kuu la Majengo unajumla ya Mita za mraba 9,273, ambapo utajumuisha maboresho ya mpangilio, mfumo wa umeme, mfumo wa maji na mzunguko wa hewa, wenye jumla ya makusanyo ya mapato milioni 204.7 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.