Waganga wafawidhi wa Hospitali zote nchini wametakiwa kujijengea uwezo wa kujitegemea katika kuboresha huduma za afya nchini kwa kuwa wabunifu katika huduma na vyanzo vya mapato ili kupunguza utegemezi wa kifedha toka Serikalini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kutembelea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma katika ziara yake ya kujionea hali ya utoaji huduma za afya zinazofanywa na hospitali za rufaa za mikoa.
"Mjenge mfumo wa kujitegemea kwani mnapaswa mambo mengine kuyafanya wenyewe katika kuendesha hospitali zenu licha ya serikali kuwapatia fedha" amesema Prof. Makubi.
Akifafanua zaidi amesema kuwa licha ya Serikali kuwapatia fedha ni wakati sasa kuondoa mtazamo huo kwani serikali itawasidia masuala kadhaa hivvo mambo mengine lazima wajitegemee ili kuacha kulalamika na kutoa huduma mbovu kwenye hospitali hizo.
Hata hivyo amewataka Waganga Wafawidhi kukaa na watumishi wote kuweza kupata mawazo ambayo wanaweza kuboresha Hospitali zao na kuweza kungoza vyanzo vya mapato na kutoa motisha kwa wafanyakazi wake.
Kwa upande wa huduma za kibingwa Prof. Makubi alielekeza viongozi wa hospitali hizo zishirikishe watumishi na jamii katika kuboresha hali ya utoaji huduma katika maeneo yao.
Vile vile Prof. Makubi ametoa muda wa miezi mitatu kwa waganga wafawidhi wote wasiokuwa wabunifu waamke na kuahidi Wizara yake itafanya tathmini na kuchuja Waganga wafawidhi wanaoendana na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wale ambao wataonekana hawafai wataondolewa.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi kushoto akipata maelezo kutoka kwa Dkt. Ernest Ibenzi kulia juu ya kifaa tiba alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma almaarufu General Hospital.
Chanzo: Ukurasa rasmi wa Instagram wizara_afyatz
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.