Na WAF, Dar Es Salaam
WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -Tamisemi itaanza kutoa mafunzo rasmi ya kuwajengea uwezo wahudumu wa Afya ngazi ya jamii 11,515 kuanzia Septemba 30, 2024 ili kufanikisha azma ya Mpango Jumuishi wa wahudumu hao na kuendeleza afua jumuishi za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Septemba 19,2024 ofisi ndogo za Wizara ya Afya NIMR Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa kwa umma juu ya kuanza rasmi kwa mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa mikoa 11 ya Tanzania Bara.
Waziri Mhagama amesema mpango huo utaanza kwenye Halmashauri 21 ndani ya mikoa 11 katika awamu ya kwanza
“Mikoa ambayo itafikiwa na huduma hii kwa Awamu ya kwanza ni pamoja na Geita, Pwani, Tanga, Songwe, Mbeya, Lindi, Tabora, Kagera, Njombe, Ruvuma, na Kigoma” ameainisha waziri Mhagama na kuongeza kuwa
“mpango huu umelenga na unahitaji kuwa na wahudumu wawili wa jinsia ke na me kila mtaa na kila kitongoji, uchaguzi wa wahudumu hao umeshirikisha wananchi na wana jamii kutoka kitongoji husika au mtaa husika.”Amefafanua Waziri Mhagama
Wakati wa utoaji wa mafunzo amesema yatatolewa kupitia Vyuo vya Afya vya Kada ya Kati kwa kipindi cha miezi sita, ambapo miezi mitatu ya awali mafunzo yatatolewa kwa njia ya nadharia na miezi mitatu iliyobaki mafunzo yatakuwa kwa njia ya vitendo katika maeneo yao ili kuongeza umahiri kwa wahudumu kuweza kutekeleza kwa uhalisia kile walichojifunza.
Waziri Mhagama amesema jumla ya wanajamii 31,275 walijitokeza kuomba nafasi huku wanajamii elfu 21,574 waliokidhi vigezo kwenye hatua ya awali walichaguliwa.
“Kwa awamu ya kwanza zoezi la kuwachagua wahudumu wa afya Ngazi ya Jamii lilifanyika kati ya tarehe 08/06/2024 hadi 25/07/2024 kwenye Halmashauri 21 kwa mikoa kumi na kuleta idadi ya waliokidhi vigezo elfu 21,574 na huku Mkoa wa Ruvuma wahudumu elfu 1,227 wanachaguliwa ili kuwa na jumla ya Wahudumu elfu 11,515 ”Amesema Waziri Mhagama
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.