Na. Dennis Gondwe, MSALATO
Wananchi wa Mtaa wa Chikole wamehamasishwa kujitokeza kushiriki zoezi la kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kuwachagua viongozi watakaowaongoza katika maendeleo.
Hamasa hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu ya hamasa ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Patrick Sebyiga alipoongoza timu hiyo kutoa hamasa kwa wananchi wa Mtaa wa Chikole, Kata ya Msalato kujitokeza siku ya kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Sebyiga ambae pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma anaeratibu Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa alisema kuwa wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura. “Mtakumbuka tumemaliza zoezi la kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, kazi iliyobaki ni kujitokeza siku ya kupiga kura tarehe 27 Novemba, 2024. Mjitokeze kuchagua viongozi wenye sifa, watakaoshirikiana nanyi katika kuleta maendeleo. Mchague kiongozi bora si bora kiongozi” aliongea Sebyiga kwa msisitizo.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeunda timu sita mahususi kwa ajili ya kuhamasisha umma kushiriki zoezi la kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tarehe 27 Novemba, 2024 chini ya kaulimbiu isemayo “Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.