Na. Aisha Ibrahim, DODOMA
MKUU wa Kitengo cha Usafi na Udhibiti wa taka ngumu Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dickson Kimaro, alisema kitengo kicho kimejipanga kikamilifu katika kuendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za udhibiti na uondoshaji wa taka ili kuhakikisha Jiji la Dodoma linakuwa katika hali ya usafi na kuvutia.
Aliyasema hayo nje ya Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la kupitia rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Akizungumzia kuhusu udhibiti wa taka ngumu, Dickson Kimaro, alisema kupitia bajeti iliyotengwa na halmashauri, kitengo hicho kinajiandaa na mchakato wa kununua mitambo maalum kwaajili ya kuchakata takataka na kuwepo kwa gari ili kukusanya na kupeleka eneo la dampo kuu la Chidaya. “Tunatarajia kwenda kununua mitambo ya kuchakata takataka, lakini kununua malori kwaajili ya uondoshaji wa taka ili kuondokana na mfumo wa ‘Collection Point’, bali kuchukua taka hizo na kupeleka dampo letu la Chidaya”, alisema Kimaro.
Aidha, aliongeza kuwa katika bajeti hiyo kutakuwa na ukusanyaji wa takwimu ya watumiaji na wazalishaji wa taka ili kubaini kiwango cha uzalishaji wa taka hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kuboresha mfumo wa ukusanyaji na uondoshaji wa taka katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma. “Tunakwenda kukusanya takwimu za watumiaji na wazalishaji wa taka, maeneo walipo na kiwango wanachozalisha kwa lengo la kuboresha mfumo wa ukusanyaji na uondoshaji wa taka katika jiji la Dodoma”, alisema Kimaro.
Nae, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Prof. Davis Mwamfupe, alisema wananchi wanatakiwa kutunza mazingira kwa kupanda miti ikiwa ni juhudi za kuunga mkono agenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya utumiaji wa nishati safi ya kupikia. “Katika kumuunga mkono mheshimwa Rais, katika adhima yake ya nishati safi tunahimizwa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti” alisema Prof. Mwamfupe.
Ukusanyaji na uhifadhi wa taka katika maeneo maalum ni njia mojawapo ya kuhakikisha maeneo mbalimbali yanakuwa katika hali ya usafi, pia kusaidia kuondokana na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.