Na. Aisha Ibrahim, MADUKANI
Wananchi wa Kata ya Madukani, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuboresha huduma za afya katika Zahanati ya Chikande na kuwahakikishia matibabu bora na karibu.
Zahanati hiyo imeboresha huduma mbalimbali zikiwemo vipimo vya maabara kama malaria, wingi wa damu, virusi vya UKIMWI na afya ya mama na mtoto ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma stahiki na elimu kuhusu lishe bora karibu na makazi yao.
Akizungumza kuhusu uboreshaji wa huduma za afya, Edina Rungwa ambae ni muuguzi katika zahanati hiyo alieleza kuwa wanatoa kipaumbele haswa kwenye huduma ya afya ya mama na mtoto kwa kutoa elimu kuhusu lishe bora na njia za kufuata ili kuepuka magonjwa katika kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua. “Kuhusu huduma ya afya ya mama na mtoto, zahanati hii tunajitahidi kwa ukubwa kuhakikisha mama wajawazito wanapata elimu ya kutosha kuhusu lishe bora na njia sahihi za kufuata ili kuepuka magonjwa mbalimbali. Hivyo, kuimarisha afya ya mtoto awapo tumboni na baada ya kuzaliwa” alisema Rungwa.
Akiongelea elimu ya lishe, alisema kuwa ni nzuri kwa mama mjamzito. “Elimu hii inamsaidia mama kujifungua mtoto mwenye afya na nguvu za kutosha, hatokuwa na shida yoyote ya maradhi. Vilevile, atazaliwa akiwa na uzito ambao ni sahihi” aliongeza.
Kwa upande wake, Pendo Edward, ambae ni mkazi wa Kata ya Madukani, alieleza kuwa kupitia kliniki ya afya ya mama na mtoto, wajawazito wanapewa elimu ya kutosha kuhusu lishe bora. “Hapa tunafundishwa kuwa mama mjamzito anatakiwa kula vizuri, kupumzika kwa wakati, kufanya mazoezi madogo madogo, kuepuka kazi nzito na kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili kujua maendeleo ya afya ya mama na mtoto aliyepo tumboni” alisema Edward.
Pia, alishukuru serikali kwa kuboresha huduma za afya katika zahanati hiyo, ikiwemo elimu ya lishe bora kwa mama na mtoto kwasababu inawasaidia kujua njia bora zakujikinga na maambukizi mbalimbali. “Tunashukuru kwa elimu hii kwasababu kwetu inatusaidia kujua ni namna gani tunaweza kutunza afya zetu hata siku ya kwenda kujifungua hatupati shida yoyote” alisema Edward.
Maboresho yaliyofanyika katika zahanati hiyo ni ukarabati wa vyumba vya madaktari, maabara na huduma ya mama na mtoto yakiwa yamesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kupata huduma bora.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.