Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WANANCHI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuacha tabia ya kufanya bahati nasibu ya kupata haki isiyostahili baada ya kuwa malalamiko yao yamekwisha tatuliwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza kutatuliwa kero na malalamiko yao kwenye Kliniki ya Ardhi inayoendelea katika siku yake ya tatu jijini hapa.
Senyamule alisema “nisisitize tunaposhughulikia kero hizi niombe wananchi wa Dodoma na kutoa wito najua kuna watu wanajirudiarudia kila wakati ambao kero zao zilishafungwa ila wanajaribu bahati nasibu nyingine. Nitoe rai wale ambao kero zao zilishafungwa huna haja ya kutumia masaa yako hapa, utapata jibu lilelile ambalo ulishalipata. Tukimaliza tatizo lako tunalifunga na tunapeana taarifa, nakala ipo kwa Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa na Kamishna msaidizi wa Ardhi”.
Akiongelea suala la utoaji hati miliki, mkuu wa mkoa alisema kuwa changamoto ya kuchelewesha hati inakwenda kukatuliwa. “Kupitia mkakati huu tunakwenda kumaliza tatizo la kuchelewesha utoaji wa hati. Kuna watu wanadai hati kwa miaka mitatu, miwili na mmoja nab ado hawajapata. Leo mnatangaziwa kwamba tatizo la kuchelewa kutoa hati limekwisha na sasa mtakuwa mnapata hati kwa wakati. Kwa sababu ya mrundikano mkubwa wa hati uliokuwepo, tumesema zoezi hili litaendelea kila mwezi, wiki moja tutakuwa tunatengeneza kliniki ya kutoa hati” alisema Senyamule.
Aidha, alisema kuwa wataendelea kusikiliza kero za wananchi. “Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inasikiliza kero, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya inasikiliza kero na Mkurugenzi anasikiliza kero. Niwahakikishie tumejipanga kwenye utatuzi wa kero za Ardhi. Tutahakikisha Ardhi haiendelei kuwa masononeko kwa wananchi wa Dodoma. Mheshimiwa Rais anafanya mambo makubwa Dodoma tunatakiwa kuyafurahia kwa Pamoja, siyo kufikiria kero za Ardhi” alisema Senyamule.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kuongea na wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri alisema kuwa kliniki hiyo itafanya kazi kwa siku tano mfululizo. Kazi hiyo ilianza juzi wananchi 1,014 walijitokeza na wananchi 514 walisikilizwa. “Kwa siku ya kwanza tuliweza kutoa hati 240 na Katibu Tawala Mkoa alikuja na kutoa hati kwa baadhi ya wananchi waliokuwepo. Wananchi waliobaki juzi tuliendelea nao jana, kulikuwa na wananchi karibu 900 na wananchi 515 kati yao walisikilizwa na hati 234 zilitolewa. Leo hati zilizoandaliwa hadi sasa zimefika 60. Nikujulishe pamoja na kutoa hati, wataalam wanasikiliza kero mbalimbali za wananchi na majibu yanatolewa na zile zinatohitaji kwenda uwandani tunaweka ahadi ya kwenda na kuzifanyia kazi” alisema Alhaj Shekimweri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.