Na WMJJWM- Dodoma
WATAALAM wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii pamoja na kada nyingine kutoka ngazi ya mikoa, halmashauri na kata nchini wametakiwa kuhamasisha jamii kuwa wazalendo, kujitolea na kuchangia katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Hayo yalisemwa jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Patrick Golwike wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wataalam kutoka ngazi ya Mikoa na Halmashauri kuhusu utekelezaji wa Mpango wa kuhamasisha na kusimamia Maendeleo Ngazi ya Msingi wa mwaka 2022/23-2025/26.
Golwike amesema Serikali inatambua mchango wa Timu ya Wataalamu ngazi ya mkoa, wilaya na kata katika kutoa huduma kwenye nyanja mbalimbali kwa jamii kwa kuandaa mafunzo hayo yatakayowezesha Mpango huo kuwafikia wataalamu waliopo kwenye maeneo yao kwa haraka.
"Natoa rai, kuwa ujuzi mtakaoupata mkautoe kwa Wataalam wa ngazi ya kata ambao ndiyo kiungo muhimu baina ya Wananchi na Serikali" amesema Golwike.
Aidha, Golwike amewaagiza wataalamu hao kwa kila mkoa kuandaa na kuwasilisha mpango kazi wa utekelezaji wa Mpango kwa kuanza kutoa mafunzo ya Mpango kwa Wataalamu ngazi ya msingi kwani bila ya kuwa na mpango kazi wa utekelezaji ni upotezaji wa rasilimali fedha na muda, kuweka mpango wa utaratibu wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi Ngazi ya msingi badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu na kujenga mazoea ya kufanya kazi kwa timu na kuwajibika ili kuwa na kazi zenye matokeo na tija.
Pia ameagiza timu za Wataalamu ngazi ya Wilaya na kata kuwezeshwa ili kuhakikisha wanafanya vikao vya kufuatilia utekelezaji wa Mpango na kufanya maboresho kwenye maeneo yanayohitaji marekebisho na kuandaa na kuwasilisha taarifa za utekelezaji.
Vilevile amesema matokeo ya kuhamasisha uzalendo kwa jamii yatafanya kuwa na Taifa linalopenda yao, jamii inayofanya kwa bidii na jamii inayojitolea katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.