RAI imetolewa kwa watakwimu wa Halmashauri, Wizara, Idara naTaasisi za umma kufanya kazi ya ziada kwa kuwapatia viongozi wao takwimu sahihi ambazo zimepata kibali kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu pale wanapowasilisha taarifa kwa wananchi au viongozi wa juu ili kuepuka upotoshaji wa takwimu.
Hayo yalibainishwa leo Novemba 21, 2023 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa wakati wa hafla ya maadhimisho ya 33 ya kilele cha siku ya Takwimu Afrika 2023 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu Tanzania (NBS) ikishirikiana na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika. ambapo hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ofisi za Takwimu zilizopo Jijini Dodoma huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma , Rosemary Senyamule.
"Watakwimu, tufanye kazi ya ziada kwa kuwapatia viongozi wetu Takwimu sahihi kwani wanaposimama mbele ya wananchi haipendezi kusikia kiongozi anataka Takwimu ambazo sio sahihi. Tuhakikishe Takwimu tunazowapatia viongozi wetu zimepata Baraka kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu kwani pale ndipo unapata Takwimu sahihi unazoweza kuzitumia sehemu yoyote," Alisisitiza Dkt. Chuwa
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa Takwimu bora ulimwenguni pia ameelezea umuhimu wa Takwimu kwa nchi za Afrika.
"Tanzania inatoa Takwimu bora zinazoaminika si Afrika tu Bali Dunia kwa ujumla. Mwaka 2010 Serikali ilitekeleza mradi wa Mpango kabambe wa Takwimu uliotekelezwa hadi mwaka 2018 na ambao uliimarisha upatikanaji wa Takwimu bora nchini, Nitoe Wito kwa Ofisi ya Mtakwimu msambaze taarifa kwenye Halmashauri zetu kwani Takwimu zinatakiwa kutumiwa kwenye kutafsiri mipango ya maendeleo kwa sekta zote. Takwimu zinasaidia nchi za Afrika kufahamu idadi ya rasilimali watu iliyopo na makundi yake,"Senyamule.
Hata hivyo, maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Kamisaa wa Sensa kwa upande wa Zanzibar Balozi Mohamed Ally Hamza ambaye amesema maadhimisho hayo yana lengo kuu la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu matumizi ya sensa pia ushirikishwaji wa jamii unasaidia kuongeza thamani ya Takwimu zetu.
Maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika hufanyika Novemba 21 kila mwaka .
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.