Rais John Magufuli amekutana (juzi) na Balozi wa China nchini, Wang Ke, Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhakikishiwa kuwa Watanzania 400 walioko katika mji wa Wuhan uliokumbwa na homa inayosababishwa na virus vya corona wote wako salama na China inafanya juhudi kubwa kuhakikisha wanakuwa salama muda wote.
Baada ya kukutana na Balozi wa China, Rais Magufuli alimkabidhi barua aliyomwandikia Rais wa China Xi Jinping, akimpa pole kwa janga la homa ya virusi vya corona lililolikumba Jiji la Wuhan na kusababisha vifo vya mamia ya watu.
Mbali na kukabidhi barua hiyo, Rais Magufuli alisema Tanzania imeguswa na kulipuka kwa janga hilo na iko tayari kutoa ushirikiano wowote ambao Serikali ya China itahitaji katika jitihada za kukabiliana na homa hiyo.
“China ni ndugu zetu, ni marafiki zetu, tunatoa pole kwa Mheshimiwa Rais Xi Jinping na Wachina wote waliopatwa na madhara ya homa hii, daima Tanzania tupo pamoja na China na katika hili tupo pamoja pia," alisema.
Balozi Wang Ke alimshukuru Rais Magufuli kwa kuguswa na janga hilo na kuungana na China katika kipindi hiki kigumu.
Alitumia fursa hiyo kueleza hali ilivyo China, akibainisha kuwa Serikali ya China imeanza kupata mafanikio katika kukabiliana na homa hiyo.
Alisema imefanikiwa kuzuia isienee katika nchi zingine kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) na nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania.
Alimhakikishia Rais Magufuli kuwa licha ya Tanzania kutokuwa na mtu yeyote aliyethibitika kuambukizwa homa ya corona, pia Watanzania 400 walioko katika Jiji la Wuhan ambao wengi wao ni wanafunzi, hawajaambukizwa homa hiyo na jitihada za kuhakikisha wanakuwa salama zinafanyika.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.